Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa na malighafi ili kurahisisha shughuli za kibiashara nchini


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo (Mb), ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa na malighafi ili kurahisisha shughuli za kibiashara nchini na kuhakikisha kina mama wanapata fursa zaidi za kiuchumi ili kusonga mbele.

Amebainisha hayo wakati akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Doto Biteko katika hafla ya Utoaji wa Tuzo za Biashara na Viwanda kwa Wanawake Tanzania 2025 (Tanzania Women Industrial Awards) inayosimamiwa na (TWCC) Machi 26,2025 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Jafo amesisitiza kuwa wanawake wanaposhiriki kikamilifu katika uchumi, taifa litaendelea kwa kasi na kusisitiza kuwa watumie fursa za masoko yaliyopo nchini na nje ya nchi kama vile Soko la SADC,EAC,AGOA na AfCFTA ambapo chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan mianya ya kufanya biashara imetanuka.

Aidha Dkt.Jafo amebainisha kuwa Serikali inakuja na mpango wa kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum wa e-Commerce kwasababu biashara Duniani ndioo ilipo.

Vilevile ametoa rai kwa Wanawake hao kuwa kama wanataka kufanikiwa zaidi kwenye biashara zao kuhakikisha Upendo, ushirikiano, na msaada ndio silaha kubwa kwani mshikamano wao ndio mafanikio yao na itawafanya kufika mbali.

Aidha Dkt.Jafo amewaasa wanawake hao kuilinda amani ya nchi iliyopo na kutoingia kwenye mambo ambayo yatahatarisha amani ya nchi.