Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya Wizara mwaka wa fedha 2021/22


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya Wizara hiyo kiasi cha TZS bilioni 105.6 kwa mwaka wa fedha 2021/22 iliyojikita katika vipaumbele 10 vinavyozingatia malengo ya kiuchumi yaliyoanishwa katika Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26, pamoja na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020.

Akiwasilisha bungeni leo Mei 22, 2021 Waziri amesema vipaumbele hivyo vimelenga katika kuendeleza, kulinda viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao mbalimbali ya raslimali zinazopatikana hapa nchini.

“Tutajikita katika kuendeleza na kulinda viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini, kuendeleza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya ngozi, nguo na mavazi” amesema.

Vipaumbele vingine ni kuhamasisha, kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma, kuendeleza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya ngozi, nguo na mavazi, kuhamasisha, kuendeleza na kulinda viwanda vya kuzalisha chuma na bidhaa za chuma.

Kuweka msukumo na mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuunganisha vifaa vya kielekroniki na magari, kuhamasisha viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi.

Pia amebainisha kuwa Serikali imejipanga katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza betri na umeme wa magari kwa kutumia rasilimali asili za nchi kama vile madini ya Lithium, Vanadium na Titanium, ambayo pia yanapatikana hapa nchi.

Vile vile tutajikita kuweka mazingira wezeshi kisera na kisheria ya kufanya biashara, kujiunga au kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika jumuiya za kiuchumi na kimasoko za kikanda kwa ajili ya kupanua fursa za kibiashara kwa bidhaa za Tanzania ambazo zitazalishwa hapa nchini.

Waziri Mkumbo ameongeza kuwa “Pia tutajikita katika kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali na wafanya biashara wadogo ili wapanue mitaji yao ili kuendesha biashara zao, tutaweka mazingira bora kisera, kisheria na kiutendaji kwa ajili ya kuchochea na kulinda ukuaji wa sekta binafsi kama injini na msingi wa ujenzi wa uchumi wa viwanda na shindani kuweza kushindana na mataifa mengine” amesema Waziri.