Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Lengo la sensa ya uzalishaji wa viwanda kwa mwaka 2025


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt.Selemani Jafo( Mb) ameelezea lengo la sensa ya uzalishaji wa viwanda kwa mwaka 2025 marejeo ya mwaka 2023 itasaidia kujua idadi ya viwanda na bidhaa zinazozalishwa kwa wingi ili kuwekewa misingi mizuri ya kisera, kikanuni na sheria Machi 20, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mhe. Jafo amesema sensa ya uzalishaji viwandani iliyofanyika mwaka 2013 ambayo ilitoa idadi ya viwanda vilivyokuwepo ni 49,243 na viligawanyika katika viwanda vidogo kabisa, vidogo, kati na vikubwa.

Waziri Jafo amekutana na wenye viwanda wa Dar es Salaam na Pwani kuzungumzia juu ya ushiriki wao pindi maofisa wa sensa watakapofika katika ofisi zao.

Amesema ushiriki wao ni muhimu kwa ajili ya kuona nchi imefikia wapi ili kuendana na wakati zitakazosaidia kupima mchango wa sekta katika uchumi nchini.

Mhe.Jafo ameongeza kuwa jambo la muhimu wanalotaka kuona kinachozalishwa na idadi ya viwanda ili kuwasaidia katika mustakabali wa maendeleo na itasaidia kwenye sera za Kiserikali inavyoweza kusaidia au kulinda viwanda.

Pia, amesema itasaidia kujua baadhi ya bidhaa zinazozalishwa kwa wingi kuwekewa misingi mizuri ya kisera, kikanuni na sheria ili kulinda viwanda nchini.

Naye, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Amina Msengwa amesema kuna mabadiliko mengi ambayo yametokea katika sekta ya viwanda kwa kipindi cha miaka 10, hivyo ni vema tukatumia fursa ya kufanya Sensa ya Uzalishaji Viwandani kwa Mwaka wa Rejea 2023 kwa lengo la kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hicho.

“Nawahikishia wamiliki wa viwanda kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, taarifa zote zinazokusanywa katika sensa na tafiti za kitakwimu ni siri na zinatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee. Katika kuhakikisha usiri wa taarifa, wadadisi baada ya kufaulu mafunzo ya mbinu za utafiti wamekula kiapo cha kutunza taarifa hizo na makosa ya kutotunza siri yana adhabu ya kifungo na faini,” amesema Dk Amina.

Amesema suala la uzalishaji wa takwimu ni jumuishi, siyo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu pekee, hivyo inahitaji ushirikiano na wadau mbalimbali katika ngazi zote za kiutawala na wananchi ambao ndiyo watoa taarifa katika sensa na tafiti mbalimbali.