Habari
Tusifanye kazi kwa mazoea- Dkt. Kijaji

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji amewataka Maafisa Biashara wa Mikoa na wakuu wa idara za viwanda biashara na uwekezaji katika halmashauri nchini kuacha kufanya kazi kimazoea.
Amebainisha hayo katika ufunguzi wa kikao kazi baina yake na Maafisa Biashara wa Mikoa na wakuu wa idara za Viwanda Biashara na uwekezaji katika halmashauri zote nchini, Aprili 06,2024 Mkoani Morogoro.
Dkt.Kijaji amesema kuwa kuwa ni wakati sasa kwa maafisa hao kuacha kujikita kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa mapato na hiyo ni kutokana na kuwa chini ya Idara ya mapato, hivyo basi amewataka kubadilika na kuwa na mtizamo mpya wa kuwa marafiki na washauri wa wafanyabiashara kwani kwa kufanya hivyo ndio kuongezeka kwa uchumi wao, mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali na hatimae kukua kwa uchumi wa Taifa.
Aidha Dkt.Kijaji ameongeza kuwa kuwa dhamira ya kikao hicho ni kupeana dondoo na uelewa wa majukumu ya Idara, namna shughuli za kisekta zitakavyoratibiwa, umuhimu wa utoaji wa taarifa pale zinapohitajika na kujipanga kwa ajili ya kutekeleza majukumu yetu katika kipindi ambapo Dunia inabadilika kwa kasi sana, ushindani mkubwa wa kibiashara na kiuchumi na Dunia kuwa kama Kijiji.
Vilevile Dkt.Kijaji ni Imani yake kuwa maafisa hao wakitoka katika kikao hicho wataweza kuwa washauri wazuri kwa Wakurugenzi, Makatibu Tawala na Wakuu wa Mikoa wao kwa masuala ya sekta wanayoisimamia, kuandaa mipango na mifumo mizuri ya utendaji kazi, kuongeza ubunifu na uharaka wa kufanya maamuzi yenye tija kwa uwekezaji, viwanda na Biashara.
Dkt.Kijaji pia ametoa pongezi kwa Taasisi ya BRELA kwa kuratibu mkutano huo ambapo elimu itakayotolewa itawafanya maafisa hao kuwa mabalozi wazuri na mfano bora kwa sehemu na Idara nyingine katika utoaji wa huduma bora na wezeshi zinazoendana na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda katika uchumi wa Dunia.
Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw.Adolf Ndunguru amesema kuwa mpango wa maendeleo wa serikali ni kuifikisha nchi katika uchumi shindani na kuboresha masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini lakini pia kuongeza tija katika uwekezaji ili mpango wa kutengeneza uchumi shindani ufanikiwe kwa kiwango kikubwa.