Habari
Uhusiano wa Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Ubelgiji unaendelea kuimarika siku hadi siku.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo (Mb) amesema Uhusiano wa Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Ubelgiji unaendelea kuimarika siku hadi siku.
Amebainisha hayo wakati anafungua Kongamano la Biashara baina ya Tanzania na Ubelgiji katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam Novemba 25,2024.
Dkt.Jafo amesema uhusiano baina ya Nchi hizo mbili umesababisha kuwepo kwa Kongamano hilo linalolenga kujadili shughuli na fursa mbalimbali zilizopo nchini na zile za Ubelgiji katika Biashara na uwekezaji.
Aidha amesema zaidi ya wawekezaji 40 wakiongozwa na Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Abook Nyamanga wamefika Nchini kwa ajili ya jukwaa hilo kwa lengo la kubadilishana fursa na urafiki na Wafanyabiashara zaidi ya 300 wa Tanzania waliohudhiria katika hafla hiyo.
Vilevile Dkt.Jafo amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kufanya uwekezaji nchini kwa kuvutia wawekezaji wengi na hiyo ndio itakiwa safari ya kuelekea uchumi wa Viwanda nchini.
Nae Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania Mhe. Peter Huyghebaert amesema mkutano huo ni matokeo ya kikao kilichofanyika mwaka 2022 kati ya Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU) mjini Brussels, Ubelgiji, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan alikutana na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Mhe. Alexander De Croo na Makampuni mbalimbali ya Tanzania na Ubelgiji kujadili namna ya kuimarisha biashara na mahusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji.