Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wadau wa Viwango wahimizwa kushirikiana na TBS katika Uandaaji wa Viwango


Wadau wa Viwango wahimizwa kushirikiana na TBS katika Uandaaji wa Viwango

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah amewahimiza wadau wa viwango nchini kushirikiana kwa karibu na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika uandaaji wa viwango ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya kimataifa.

Aidha amewaalika wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini kushiriki katika mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini yenye kauli mbiu ya "Kuwawezesha Walaji kupitia Uandaaji wa Viwango ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma bora na Salama ambayo yanalenga kuwapata washindi katika ngazi ya kitaifa ili waweze kushiriki katika ngazi ya kikanda na hatimaye kupata mshindi katika bara la Afrika kwa ujumla.

Dkt. Abdallah alitoa wito huo Novemba 30, 2023 wakati akizungumza katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani 2023 kwa Tanzania yaliyofanyika Makao Makuu ya TBS, Ubungo, Dar es Salaam

"Viwango ni muhimu katika kuendeleza sekta ya viwanda na biashara nchini. Tunafahamu kuwa ubora wa bidhaa yoyote inayozalishwa nchini na nje ya nchi inahitaji uwepo wa kiwango husika ili kuweza kukidhi matakwa ya mazingira, afya ya walaji, usalama na ustawi wa jamii yetu," alisema Dkt. Abdallah.

"Kwa hiyo, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wadau wote wakiwemo taasisi za elimu ya juu, taasisi za utafiti, mashirika ya umma, wadau wa maendeleo, wazalishaji, wajasiriamali na vyama vya kisekta kwa kuendelea kuandaa viwango kwa ufanisi mkubwa," alisema Dkt. Abdallah.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya, alisema kuwa maadhimisho hayo ni muhimu kwani yanalenga kuamsha uelewa miongoni mwa wafanyabiashara, wenye viwanda na walaji kuhusiana na umuhimu wa viwango katika kuboresha bidhaa na huduma katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

TBS, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imefanikiwa kuandaa viwango zaidi ya 4,000. Viwango hivi ni pamoja na vile vinavyobainisha matakwa ya usalama, matakwa ya utengenezaji, matakwa ya matumizi pamoja na kanuni za upimaji.