Habari
Wahitimu wa CBE waaswa kutumia mitandao ya kijamii kujiajiri

Wahitimu wa CBE waaswa kutumia mitandao ya kijamii kujiajiri
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ametoa wito kwa wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kutumia mitandao ya kijamii kupata ajira badala ya kutumia mitandao hiyo kufanya mambo yasiyofaa.
Kigahe ametoa wito huo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb.) wakati wa mahafali ya 58 ya CBE- Kampasi ya Mwanza katika Ukumbi wa R.Meridien Park 25 Novemba, 2023
Aidha Kigahe amewaasa wahitimu hao kuwa elimu waliyoipata ikawe chachu ya kwenda kuanzisha biashara ili waende kujiajiri na kuajiri Watanzania wengine.
"Kamwe msiende kuwa sehemu ya kulalamika kuhusu ukosefu wa ajira bali mkawe suluhisho la ukosefu wa ajira kwa kutumia elimu mliyoipata" Amesema Kigahe
Aidha Kigahe amesema Serikali itashughulikia changamoto zinazokikabili Chuo hicho ikiwemo
upungufu wa mabweni,uzio na barabara pamoja na uhaba wa fedha ili Chuo hicho kiendelee kuoa elimu kwa wanafunzi wengi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa CBE , Prof. Wineaster Anderson katika hotuba yake akimkaribisha mgeni rasmi ameeleza kwamba mwaka 2023 CBE imetoa wahitimu 2443 waliohitimu kutoka Kampasi 4 za Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Mbeya.
Aidha amefafanua kwamba kati ya wahitimu hao 1226 wanatoka Kampasi ya Dar es salaam, 792 Kampasi ya Dodoma, 261 Kampasi ya Mwanza na 164 Kampasi ya Mbeya
Aidha Prof. Wineaster ameeleza pia changamoto zinazokikabili Chuo hicho Kampasi ya Mwanza kuwa ni ukosekanaji wa uzio na mindo mbinu ya hostel za wanafunzi kwani wanafunzi wengi katika Kampasi hiyo wanakaa nje ya chuo.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe Dkt. Merdad Kalemani ( Mb) amewaasa Wahitimu CBE kuitumia Elimu waliyoipata vyema kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upende wake Mkuu wa Chuo cha CBE Prof. Edda Lwoga emeelezea kuwa uanzishwaji wa programu mbalimbali Atamizi za Biashara ( Business Incubators) pamoja, (Apprenticeship Training) na clinic ya Biashara kwa ajili ya wajasiriamali na wafanyabiashara zinalenga kuwajengea uwezi wajasiliamali wengi ili waweze kuanzisha na kukuza biashara zao kwa tija.