Wana Njombe changamkieni fursa za miradi ya viwanda vinavyoanzishwa
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Seleman Jafo (Mb) amewataka Wananchi wa Mkoa wa Njombe kuchangamkia fursa ya miradi ya viwanda inayojengwa katika maeneo yao ili kuongeza ajira kukuza biashara na uchumi kwa ujumla.
Vilevile amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikino na kuwalinda Wawekezaji ili kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini na kutimiza dhamira ya Rais Samia Suhuhu Hassan katika kukuza uchumi.
Waziri Jafo ameyasema hayo Februari 19, 2025 mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuchakata
Chuma cha Fujian na Kiwanda cha kuchakata mafuta ya Parachichi Avo Africa vilivyopo Makambako Mkoani Njombe kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi na shughuli za uzalishaji.
“Kwa hiyo wananchi tujiandae na mradi huu, wakinamama ntilie hakikisheni mnachukua fursa ya kuwapikia chakula lakini pia wakinababa mchukue fursa hiyo ya kuhakikisha mnashiriki shughuli za hapa,” amesema Waziri Jafo.
Aidha, Waziri Jafo ameutaka Mkoa wa Njombe kuwa Mkoa wa Mfano wakati wa Utekelezaji wa Programu ya Viwanda 2025 - 2030 kwa kila Mkoa kwa lengo la kuongeza ajira, Pato la Taifa na kukuza uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema Mkoa huo umejipanga kuwa wa kwanza katika kuweka mazingira bora na nafuu katika kuvutia na kuwapokea wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya viwanda katika Mkoa huo.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Avo Africa Bw. Nagib Karmal ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwaunga mkono wawekezaji, kuwapa uhuru pamoja na amani na usalama kwa sababu bila hivyo huwezi kufanya biashara.