Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wananchi wa Wilaya ya Kilwa kushikamana na kusimamia Miradi ya Maendeleo


Mhe Dkt Selemani Jafo (Mb) amewashauri Wananchi wa Wilaya ya Kilwa kushikamana na kusimamia Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa Wilayani humo ikamilike kwa wakati na iendane na gharama halisi ili kutimiza Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha Wananchi hao wananufaika na kuliletea Taifa maendeleo ya kijamii, kiichumi na kosiasa kwa ujumla.

Ameyasema hayo Septemba 17, 2024 wakati wa Ziara Maalum Kilwa, Mkoa wa Lindi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na kuongea na Wananchi wa Maeneo hayo ikiongozwa na Kauli Mbiu isemayo "Rais Samia na Maendeleo Wasikie na Waone" iliyoanza tarehe 17 - 21/09/2024.

Akiwa Wilayani humo katika Mradi wa Nyumba za Walimu (Two in one) katika Kata ya Somanga ameliagiza TANESCO kuhakikisha nyumba hizo zinapata umeme na TARURA kuhakikisha inajenga barabara ndani ya miezi miwili (2) ili kuweka mazingira bora ya kuishi na kufanya kazi kwa ufanisi kwa Walimu hao.

Vilevile, Dkt Jafo aliielekeza Mamlaka ya Maji Kilwa Masoko (KIMUWASA) inayosimamia Mradi wa maji katika vijiji vya Mavuji, Nangurukuru, Singino, Kivinje, Mpara na Masoko uliopo Kilwa kuandaa Mpango unaonesha Mradi huo utakamilika lini na kuwasilisha katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi ndani ya Wiki mbili (2) ili kuhakikisha Mradi huo unaleta manufaa yanayotarajiwa.

Aidha, Dkt Jafo amebainisha kuwa ujenzi wa Mradi wa Bandari ya Uvuvi unaolenga kurahisisha upatikanaji wa Samaki, Soko na kukuza biashara uchumi kwa ujumla pamoja ujenzi wa Kituo cha Afya cha Njinjo, Kipimimbi unaendelea kwa kasi , unaendana na gharama iliyopangwa na hivyo kufikia malengo yanayotarajiwa.

Akiongea na Wananchi wa Kipimindi Wilayani Kilwa Dkt Jafo amewapongeza wananchi wa Wilaya hiyo kwa kutumia Mfumo wa stakabadhi gharani hususani katika mazao ya ufuta na mbaazi na kupata mafanikio makubwa katika kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe Zainab Telack ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani humo inayolenga kuleta manufaa makubwa kwa Wananchi wa Mkoa huo na kuwaomba kutumia fursa za miradi hiyo ili kuleta maendeleo ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.