Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wazalishaji wa bidhaa Nchini kuweka kipaumbele suala la ubora wa bidhaa kwani ndio ajenda muhimu kwa kutengeneza uchumi wa nchi


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Selemani Jafo (Mb) ametoa rai kwa Wazalishaji wa bidhaa Nchini kuweka kipaumbele suala la ubora wa bidhaa kwani ndio ajenda muhimu kwa kutengeneza uchumi wa nchi.

Ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Ubora Duniani na Utoaji wa Tuzo za Kitaifa za Ubora kwa washindi wa msimu wa tano 2024 yaliyofanyika katika ukumbi wa PSSSF Tower Jijini Dar es Salaam.

Dkt.Jafo ameyataka makampuni mbalimbali kujua kuwa mashindano hayo yanalenga kuchochea uzalishaji wa bidhaa kwa kuzingatia ubora ili kuweza kufikia viwango vya masoko ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Aidha amesema kuwepo kwa vyakula na vifaa mbalimbali vinavyokosa ubora husababisha madhara makubwa kwa kutengeneza watu wenye magonjwa pamoja na madhara kwenye miundombinu mikubwa inayotumia vifaa vya ujenzi ambavyo havina ubora.

Pia ametoa rai kwa Wajasiliamali kutumia fursa kujenga biashara na ujasiliamali wao ili wakue na kuanza kutengeneza bidhaa zinazokidhi Viwango kwani fursa iliyopo ni wajasiliamali wadogo wanalelewa na SIDO na ndani ya miaka mitatu husaidiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) bila gharama.

Pamoja na hayo Dkt.Jafo amewataka watanzania wawe na tabia ya kutumia bidhaa za ndani kwani uwekezaji wa viwanda umekuwa mkubwa na bidhaa nyingi zinazalishwa nchini na kwakufanya hivyo inahamasisha uwekezaji kuwa mkubwa.

Vilevile ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania kujenga uelewa na kuitangaza siku hiyo ya Viwango kwa kiasi kikubwa zaidi kwa Watanzania ili kuwa na idadi kubwa ya washiriki kwenye tuzo zijazo katika vipengele tofauti.