Habari
Waziri Jafo akabidhi Magari matano kwa Wakala wa Vipimo
WAZIRI JAFO AKABIDHI MAGARI MATANO KWA WAKALA WA VIPIMO
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amekabidhi magari matano kwa taasisi ya Wakala wa Vipimo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za uhakiki na ukaguzi wa vipimo bidhaa zilizofungashwa kwa haraka na kwa wakati kwa Wananchi ambao ndio watumiaji wa vipimo na bidhaa kila siku.
Dkt.Jafo ameelekeza magari hayo yakatumike katika kaguzi mbalimbali za bidhaa zilizofungashwa kwa kuhakikisha vipimo vinakuwa sahihi katika bidhaa za nondo na mabati kwa kusimamia usahihi wa vipimo ili mnunuzi wa mwisho aweze kupata bidhaa inayoendana na thamani ya fedha anayolipa.
Aidha Dkt.Jafo amewaagiza wazalishaji wote wa nondo kuzalisha nondo zenye ubora na zenye vipimo sahihi halikadhalika kwa wazalishaji wa mabati kwani l Wananchi wananunua nondo ambazo hazina ubora kiasi kwamba hata majengo yao yanakuwa hatarini kwakuwa wazalishaji wanasema wanazalisha nondo za mm 16 lakini zinakuwa chini ya vipimo hivyo.
Waziri Jafo ameielekeza wakala wa Vipimo kuendelea kufanya kaguzi za kushtukiza kwenye viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za nondo na mabati ili kuhakikisha bidhaa zinazofika kwenye masoko zinakuwa na vipimo sahihi kwa lengo la kuwalinda wanunuzi wa bidhaa hizo ili kuepukana na uchezewaji wa vipimo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo(WMA) Bw. Alban Kihulla amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 Wakala ilipanga kununua magari saba lakini mpaka sasa imepokea magari matano ambayo ameyakabidhi leo na magari mengine mawili yatafika hivi karibuni.
Bw. Alban amesema Wakala wa Vipimo itaendelea kutoa huduma za usimamizi wa vipimo kwa wakati kwa lengo la kuwalinda watumiaji wa huduma hizo na kaguzi mbalimbali za kushtukiza zitaendelea kufanyika ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia kwenye masoko zinakuwa na vipimo sahihi na adhabu kali zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 kwa wazalishaji watakaobainika kuchezea vipimo.