Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Waziri Mkuu awahimiza wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewahimiza wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini katika maeneo yote ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) kwa kuwa Serikali inachukua hatua madhubuti katika kuboresha utoaji wa huduma na utunzaji wa mazingira ili kuvutia wawekezaji nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo, Juni 18, 2021 wakati alipofanya ziara katika eneo la EPZA lililopo wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam na alitembelea baadhi ya Viwanda vilivyopo katika eneo hilo.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kusimamia (EPZA) katika kuboresha utendaji kazi ikiwemo kufanya mabadiliko ya watumishi, utunzaji wa mazingira na majengo yaliyopo katika eneo hilo na utoaji wa huduma hususani utoaji wa vibali vya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji  ambao wataongeza ajira na pato la taifa.

 “Kampuni 18 zilizoomba kuwekeza katika eneo hili zilikataliwa kwa sababu ya urasimu uliopo hapo EPZA. Mwaka 2020 kampuni 18 ziliomba leseni kwa ajili ya uwekezaji katika eneo hili lakini kati yake kampuni tano tu ndio zilipewa leseni, wengi walionekana hawana sifa….vikwazo vingi ni urasimu tu.”

Aidha, aliwataka watumishi wa Mamlaka hiyo kubadilika na kufanya kazi kwa  weledi, ubunifu na uzalendo katika kuhakikisha malengo ya uanzishwaji wa  Mamlaka hiyo yanafikiwa kwa kuongeza wawekezaji katika maeneo ya EPZA ambao watachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la aiira, teknolojia na pato la taifa na huvyo kukuza uchumi wa nchi.

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb), aliahidi kutekeleza maelekezo yote yalitolewa na alieleza hatua mbalimbali ambazo Wizara yake imechukua katika kuboresha utendaji kazi wa mamlaka hiyo ili kuboresha huduma na kuvutia wawekezaji ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa Maeneo ya EPZA yaliyopo Kurasini, Bagamoyo, Mtwara na Ruvuma.

Naye Waziri wa Nishati Dkt. Merdard Kalemani alisema atahakikisha kuwa kuna umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo yote ya EPZA na kuwahimiza wawekezaji waendelee kuwekeza katika maeneo hayo.

Aidha, katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya Viwanda vilivyopo EPZA ambavyo ni Kiwanda cha Kushona suruaji za cha Tooku ambacho soko kubwa la bidhaa zake liko nchini Marekani kwa nguo aina ya jeans. Kiwanda kingine ni kiwanda cha nafaka cha Somani na Kiwanda cha DIZ Card kinachotengeneza kadi za aina mbalimbali.

Pia, Waziri Mkuu alifanya ziara katika Kampuni Africab Group Tanzania kinachojihusisha na utengenezaji wa vifaa vya umeme kama transfoma na nyaya za umeme kilichopo Kurasini na kuipongeza kwa uwekezaji mkubwa ilioufanya katika sekta ya nishati nchini. Aidha, walielezea kuwa wameanza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Dawa za Binadamu kitakacho julikana  kama Cure Afya  Pharmaceuticals Limited kitatengeneza dawa za aina mbalimbali kama za vidonge, maji na maji tiba Kimbiji.

Waziri Mkuu amesema uzalishaji huo umekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijiji kwani kabla ya kampuni hiyo kuanza uzalishaji wa bidhaa hizo nchini Serikali ilikuwa inatumia gharama kubwa kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa  aliambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Prof.Kitila Mkumbo pamoja, Waziri wa Nishati Mhe.Dkt.Medard Kaleman na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.