Habari
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo amewaagiza wakuu wote wa Mikoa Nchini kuhakikisha wanatenga maeneo ya Viwanda kwa kuwa atahakikisha anahamasisha wawekezaji na wafanyabiashara wengi zaidi kuja Nchini.
Dkt. Jafo ametoa agizo hilo alipotembelea kiwanda kinachozalisha waya, sufuria na kurejesha betri za magari na pikipiki cha Balochistan Group of Industry (BGI) kilichopo Wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani ambacho huchangia kodi ya serikali ya sh milioni 600 kwa mwaka.
Amesema kuwa serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji katika Nyanja mbalimbali kuwekeza nchini, ni muhimu kwa wakuu hao wa Mikoa kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo kwa kutenga maeneo zaidi ili kurahisisha uanzishwaji wa viwanda mbalimbali kwenye maeneo hayo Pamoja na kuwataka wenye viwanda kufahamu kuwa , wamekuwa msaada mkubwa kwenye ajira na ajira ni jambo la msingi hivyo ni lazima kuhakiisha wanaangalia maslahi ya wale wanaowasaidia kufanya kazi katika maeneo yao.
Amesema kuwa kwa taarifa alizonazo kiwanda hicho kina vijana takriban 200-300 walioajiriwa ambao wamekuwa wakipata mkate wao wa kila siku, juhudi ambazo zimefanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Dkt.Jafo amesema kuwa Serikali itatoa mianya yote ya kuhakikisha uwekezaji unarahisishwa Nchini hivyo wawekezaji wendelee kufanya jitihada za kuwekeza na lengo ni kupata viwanda vingi ili kuongeza ajira nyingi zaidi kwa vijana.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BGI, Ndg.Khudadad Bizanto ameshukuru Serikali ya Tanzania kwa jitihada za uboreshwaji wa mazingira ya biashara nchini na kwamba ana mpango wa kuongeza kiwanda kingine cha betri pamoja na nyaya mbalimbali kitakachofikisha idadi ya waajiriwa 3000 Pamoja na kuongeza Kiwanda cha mafuta Mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mhe. Hadija Nasri amesema kama Wilaya wana imani kuwa sekta ya viwanda itaendelea kuimarika na kwamba Mkuranga ina viwanda 128, ambapo ni miongoni mwa eneo ambalo uwekezaji wa viwanda ni mkubwa zaidi kuiomba serikali kutoa uangalizi wa pekee kwa wilaya hiyo haswa kwenye miundombinu ili kuvutia zaidi wawekezaji.