Habari
Witowatolewa kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga kutumia Jukwaa la Biashara la Mkoa huo
-
-
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah ametoa wito kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga kutumia Jukwaa la Biashara la Mkoa huo katika kuongeza uelewa juu ya Sera,Sheria na taratibu za Biashara ili ziweze kusaidia katika ufanyaji wa biashara.
Dkt.Hashil ameyasema hayo katika hotuba yake kwaniaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) katika Jukwaa la Biashara Mkoani Shinyanga lililofanyika Novemba 25,2023 katika Viwanja vya Karena Hotel Manispaa ya Shinyanga.
Aidha amesema kuwa kufanyika kwa Jukwaa hilo ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye anaifungua Nchi na anayeweka Mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara na uwekezaji Nchini.
Vilevile amebainisha kuwa kwa umuhimu wa Jukwaa hilo imempendeza Mhe. Dkt. Kijaji kuzielekeza baadhi ya Taasisi za Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Wakala wa Vipimo (WMA) na TBS Shirika la Viwango Tanzania(TBS) kutoa mada za kuelemisha juu ya kusaidia mazingira wezeshi ya ufanyaji Biashara kwa Wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Jukwaa hilo Ndg.Jonathan Kifunda amesema kuwa Jukwaa hilo ni la siku tatu kuanzia Novemba 24-26 Novemba,2023 na limehusisha Wafanyabiashara wakubwa na kati,Wajasiliamali,Wakulima na Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Shinyanga.