Habari
ZIARA YA RAIS SAMIA NCHINI BURUNDI YAZAA MATUNDA YA UJENZI WA KIWANDA DODOMA CHA DOLA ZA MAREKANI MILIONI 180
Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Burundi iliyofanyika mwezi Julai Mwaka huu imezaa matunda ya Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea cha cha Itracom Fertilizer Limited kinachojengwa eneo la Viwanda Nara jijini Dodoma ambapo ujenzi umefikia asilimia 35 na utagharimu Dola za Kimarekani milioni 180 na kuajiri wafanyakazi wa kudumu takriban 3000 na kitakuwa na uwezo uliosimikwa wa kuzalisha mbolea tani 500,000 kwa mwaka.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo Oktoba 12, 2021 alipoambatana na Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Antony Mtaka kufanya ziara ya kutembelea na kukagua viwanda na miradi inayosimamiwa na Wizara katika Mkoa wa Dodoma ambapo ametembelea Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited, eneo la kongano la viwanda Zuzu, kiwanda cha Mafuta ya kula cha Pyxus Agriculture Tanzania limited, Kiwanda cha Mabati cha Dragon Limited na Kiwanda cha Dane Holdings Limited.
“Ujenzi wa Kiwanda hiki cha Mbolea ni Matunda ya ziara ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Burundi, tulipotembelea Burundi Mheshimiwa Rais alikuta kiwanda cha mbolea ya asili cha Itracom Fertilizer Limited ambacho ni kiwanda kikubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na moja ya mazungumuzo ni kuwa kile kiwanda kijegwe pia hapa Tanzania na mara moja wawekezaji hawa walikubali kuja kujenga kiwanda hapa Dodoma na tumeona wameshaanza ujenzi hata kabla ya taratibu za kawaida za uwekezaji kukamilika” ameeleza Prof. Mkumbo
Prof. Mkumbo amesema kuwa Tanzania hakuna kiwanda cha mbolea kikubwa kinachotosheleza mahitaji na hiyo imeleta adha kubwa kwa wakulima na Serikali kutokana na bei ya mbolea kupanda katika soko la dunia zaidi ya mara tatu, kwahiyo ujenzi wa kiwanda hiki utakuwa mkombozi kwa kuwa na mbolea ya uhakika kwa sababu kitazalisha mara nne ya kiwanda cha Burundi na kinategemewa kukamilika ifikapo mwezi wa nane mwaka 2022.
Amesema kuwa katika mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano lengo kubwa ni kuzalisha ajira milioni nane na kiwanda hiki kitazalisha ajira 3,000 za kudumu na ajira zisizo za kudumu Zaidi ya 8,000 hivyo amewasihi wananchi wa Dodoma kutumia fursa hiyo maana moja ya changamoto katika ujenzi wa kiwanda hicho ni vibarua kutokuwa na desturi ya kufanya kazi kwa kujituma jambo lililolazimu kuchukua vibarua kutoka mikoa mingine.
Aidha, Prof. Mkumbo baada ya kutembelea kiwanda cha Mafuta ya kula cha Pyxus Agriculture Tanzania limited na Kiwanda cha mvinyo cha Dane Holdings Limited vinavyotegemea malighali kutokana na kilimo ameeleza kuwa katika mpango wa Maendeleo na Ilani ya Chama cha Mapinduzi mkazo mkubwa umewekwa kwenye kufungamanisha Kilimo na Viwanda na changamoto kubwa iliyopo ni uzalishaji mdogo kwenye kilimo unaosabisha uzalishaji mdogo kwenye viwanda, hivyo kazi kubwa ni kuweka mkazo na msisitizo kwa wakulima kuzingatia kilimo bora na chenye tija.
Vilevile, Prof. Mkumbo ametoa wito kwa Benki zilizopo nchini kujikita kuwasaidia wajasiliamali wenye viwanda vidogo kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu na kuwalea mpaka pale watakapoona wanaendelea kukua na kuweza kujiendesha wenyewe pia akawelekeza SIDO kuendelea kuwasaidia na kutatua changamoto zao ndogo ndogo kama yalivyo majukumu yao.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Antony Mtaka ameeleza kuwa Ujenzi wa kiwanda cha mbolea ukikamilika utaweza kuinua uchumi wa Dodoma kwa kulipa kodi na Maisha ya Wananchi kwa kupata ajira nyingi na itasaidi kilimo cha Zabibu kinachohitaji Mbolea na kwenye mazao mengine vilevile ametoa wito kwa vijana wa Mkoa wa Dodoma kuwa na utamaduni wa kujituma kufanya kazi.
Vilevile, Mhe. Antony Mtaka ameeleza kuwa zao la Zabibu ndio utambulisho wa Mkoa wa Dodoma na ndilo eneo pekee duniani ambapo zabibu inalimwa kwa misimu miwili kwahiyo likilimwa kwa tija itaweza kuitangaza nchi,litainua uchumi wa wakulima pia litakuwa zao la ufahari linalotambulisha makao makuu ya nchi yetu.
Nae, Msimamizi mkuu wa Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea cha cha Itracom Fertilizer Limited, Bw. Rubenga Samson ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira Mazuri na vivutio vya kufanya uwekezaji nchini kwa kuwapelekea umeme na mahitaji mengine huku akiomba kuongezewa maji ambayo kwa sasa wanapata asilimia 10 ya mahitaji katika eneo la uwekezaji.