Habari
BRELA yakutana na kamati ya kudumu ya bunge ya viwanda, biashara na mazingirana kutoa taarifa ya majukumu yao

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa elimu ya Majukumu yao kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika ukumbi wa Bunge leo tarehe 18/01/2020. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na BRELA. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa kuhusiana na kazi na shughuli zinazofanywa na Wakala katika kutoa huduma kwa jamii bila kusahau changamoto mbalimbali zinazoikabili BRELA ili Kamati iweze kushauri. Katika mawasilisho yaliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Brela Bi. Roy Mhando alieleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na wakala ambazo ni kusimamia Sheria ya Makampuni Sura ya 212, sheria ya majina ya biashara sura ya 213, sheria ya alama za biashara na huduma, Sheria ya Usajili wa Hataza, Sheria ya Leseni za Viwanda, Sheria ya Leseni za Biashara. Ameileza Kamati kuwa Wakala inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inatimiza majukumu yake kwa ufasaha na kuwafikia wateja wake kwa kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari. Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Kanali mstaafu Masoud Ally Khamis (Mb) amempongeza Kaimu Afisa mtedaji Mkuu wa Wakala kwa kazi nzuri anayoifanya na kuitaka Wakala kuendelea kutoa Elimu ili wadau wa biashara wajue huduma mbalimbali wanazotoa hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo wadau wa biashara hawajui umuhimu wa kurasimisha biashara zao pia hawana uelewa wa matumizi ya Tehama. Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb) amewashukuru Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa maoni na mawazo yao waliyoyatoa ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ya kuongeza ufanisi kiutendaji katika kuwahudumia wananchi pia ametoa maelekezo kwa BRELA kuwa waweke mkakati wa mawasiliano wenye lengo la kutangaza huduma zinazotolewa na Wakala kupita vyombo mbalimbali vya habari hasa kupitia redio za kijamii. Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndasa ameipongeza BRELA katika suala zima la kuwahudumia wateja kwani wamewawezesha wananchi wengi kupata huduma kwa urahisi kwani hivyo ndivyo inavyotakiwa katika kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe amewashauri BRELA wawemakini kwenye kazi za kila siku ili kuondoa malalamiko na changamoto wanazopata wateja hii itasaidia kuongeza idadi ya wateja na pato la Taifa kwa ujumla. Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Hawa Mwaifunga ameiomba BRELA wafike katika wilaya na Mikoa mbalimbali hapa nchi kwani huko kuna wadau wengi wanaohitaji kujua faida za kurasimisha biashara zao. Mbunge wa Monduri Julius Kalanga Laizer ameipongeza BRELA kwa kuandaa mfumo wao ambao wanaendelea kuuhuisha na akapendekeza ni vema taasisi zingine za biashara kuunganishwa pamoja. Pia, amewapongeza watumishi wa BRELA kupitia kitengo cha TEHAMA wanaotoa msaada kwa wateja katika matumizi ya mtandao wa BRELA kwani wamekuwa wakisaidia sana wananchi pale wanapopata changamoto. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Kanali mstaafu Masoud Ally Khamis (Mb) alihitimisha kikao kwa kuwashukuru wajumbe wa kamati hiyo na kuwahimiza kuendelea kuishauri vema Serikali ili kuweza kufikia adhima ya Uchumi wa Kati unaongozwa na Viwanda ifikapo 2025.