Habari
UWEZESHAJI BIASHARA NI KIPAUMBELE KIKUBWA KWA SERIKALI
Serikali imesema kuwa masuala ya uwezeshaji biashara ni moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ya Awamu ya Sita iliyo chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Balozi Waziri Salum wakati akifungua Mkutano wa Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Biashara (National Committee on Trade Facilitation-NCTF) Ngazi ya Uongozi (Steering Committee) uliofanyika Agosti 13,2026 Jijini Dodoma.
Balozi Salum amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuweka mazingira wezeshi ya biashara nchini pamoja na biashara za Kikanda na Kimataifa hivyo kufikia lengo hilo Tanzania imeridhia mkataba wa Uwezeshaji wa Biashara wa Kimataifa (Trade Facilitation Agreement – World Organization Organization TFA - WTO) ambao umeweka mazingira, taratibu na miongozo ya ufanyaji biashara ya kuuza bidhaa nje ya nchi (export), kuingiza bidhaa nchini na kupitisha bidhaa (import) kwenda nchi jirani (transit).
Aidha amesema katika uwezeshaji biashara Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi kama barabara, reli, viwanja vya ndege, upanuzi wa bandari na uboreshaji wa miundombinu ya ubora na usalama, matumizi ya mifumo ya kieletroniki na uboreshaji wa huduma za mawasiliano.
Katika kutambua umuhimu wa uwezeshaji biashara katika kuleta mabadiliko yatakayoiwezesha Tanzania kuwa sehemu bora ya kufanya biashara na kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla amewataka wajumbe hao wanatimiza wajibu ndani na nje ya Kamati ili kuweza kufikia malengo kwa nchi yetu.
Mkutano huo pia uhusisha Kamati hiyo yenye wajumbe kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambazo zitajadili namna ya kutekeleza mkataba huo pamoja na kuishauri Serikali masuala mengine ya biashara ili kuendelea kunufaika na fursa za biashara katika ukanda wa EAC, SADC na Soko Huru la Biashara Afrika (EfCFTA).
