Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MAAFISA BIASHARA WATAKIWA KUIBUA FURSA ZA UWEKEZAJI, KUONGEZA THAMANI


Serikali imewataka Maafisa Biashara nchini kutumia nafasi zao kikamilifu kuibua fursa za uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao na kuboresha mazingira ya biashara katika halmashauri, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Wizara Mhe. Judith Kapinga (Mb) wakati wa Kikao cha Tatu cha Wizara ya Viwanda na Biashara na Maafisa Biashara nchini, kilicholenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao katika kukuza biashara, viwanda na uwekezaji Agosti 17, 2026 jijini Dodoma.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa viwanda katika Afrika Mashariki na Kati, ikiwamo kufikia uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza kipato cha Mtanzania hadi dola 7,000. Amesema kufikia malengo hayo kunahitaji uchumi imara, jumuishi na shindani unaotegemea sekta binafsi, sayansi na teknolojia, uwekezaji, utafiti pamoja na nguvu kazi yenye ujuzi.

Hata hivyo ametolea mfano wa mahindi, amesema wakulima wanapaswa kusaidiwa kuondokana na kuuza mazao ghafi na badala yake kuzalisha bidhaa kama unga wenye chapa na kuufikisha kwenye masoko, hatua itakayoongeza kipato na kuchangia kupunguza umaskini.

Aidha, amesema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kushirikishwa kikamilifu katika uzalishaji, uwekezaji na biashara kupitia fursa za mikopo na uwezeshaji. Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, viwanda vikubwa vipya 25 vilijengwa katika sekta mbalimbali na kutoa ajira 39,000, zikiwamo ajira 7,600 za moja kwa moja na 31,000 zisizo za moja kwa moja.

Katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji, Londo ameitaka mikoa kuhuisha kanzidata za viwanda, biashara, masoko, leseni, wawekezaji na maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kiuchumi, huku kila halmashauri ikiandaa wasifu wa fursa za uwekezaji unaoonyesha upatikanaji wa malighafi, miundombinu, masoko na maeneo ya uwekezaji.