Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

CBE yatakiwa kutoa Elimu inayokidhi mahitaji ya Soko la ndani na kimataifa


CBE yatakiwa kutoa Elimu inayokidhi mahitaji ya Soko la ndani na kimataifa

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Dkt. Selemani Jafo (Mb.) ameisisisitiza Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kusimamia taaluma ili Wahitimu wa Chuo hicho waweze kutumia fursa zilizopo katika Soko la Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Mpango wa Ukuaji na Fursa wa Afrika (AGOA), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na kutimiza malengo ya Dira ya 2075 katika sekta ya viwanda na biashara,

Vilevile Dkt. Jafo ameielekeza kwa Bodi hiyo kuhakikisha Watumishi wa Chuo hicho wanafanya kazi kwa weredi, ushirikiano, upendo na uadilifu ili kuhakikisha vijana wanapata elimu bora ya biashara mara kwa mara katika mafunzo ya muda mfupi kwa kuwa CBE ina dhamana ya kuwapa maarifa wafanyabiashara nchini kuhusu namna bora ya kushiriki kwenye biashara ya kimataifa

Waziri Jafo ameyasema hayo Februari 10,2025 wakati wa akizindua Bodi ya Uongozi wa CBE jijini Dar es salaam, ambapo alikitaka Chuo hicho kujitangaza nje ya mipaka ya Tanzania ili waweze kupata wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali badala ya kutegemea wanafunzi wa ndani pekee kwani taaluma inayotolewa chuoni hapo inakidhi vigezo vya kimataifa.

Aidha, alikitaka Chuo hicho kinawajibu wa kuandaaa vijana mahiri wanaoweza kushiriki kwenye biashara za kitaifa na kimataifa wakiwa na ujuzi uliokamilika utakaowawezesha kumudu kushindana na wenzao kimataifa ikiwemo kuandaa programu za muda mfupi kuhusu masuala ya uongozi katika biashara, namna ya kufanya usahili wa kazi, kuandika barua ya kuomba kazi kwa wiki moja au mbili ili kutoa maarifa ya kuwa mahiri kwenye sekta ya biashara.

Akimkaribisha Waziri kuzindua Bodi hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hashil Abdallah, ameisisitiza Bodi hiyo kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya soko na ushindani wa kibiashara ili kukuza sekta ya viwanda na biashara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya CBE, Prof. Zacharia Mganilwa, aliahidi kuwa Bodi hiyo itashirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuhakikisha mbinu mbadala za kuimarisha elimu ya biashara zinatumika kwa ufanisi.