Habari
SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAFANYABIASHARA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya Biashara kwa kutatua changamoto za wawekezaji na kuweka mifumo rafiki ya kuharakisha ukuaji wa Uchumi na Biashara.
Dkt. Abdallah ameyasema hayo kwenye Kikao cha Mkutano wa Tisa wa Baraza la Biashara na Uwekezaji Songwe Novemba 28, 2025 mkoani humo.
Dkt. Abdallah ameongeza kuwa Wizara na Taasisi zilizo chini yake zimejipanga sawasawa kuhakikisha zinawafikia wafanyabiashara popote walipo na kushughulikia changomoto zao kwa usahihi, haraka na kwa ufanisi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabari Makame amesema kuwa
Serikali mkoani Songwe imetangaza mpango kabambe wa kuanzisha maonesho makubwa ya biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani wa mkoa huo katika kuvutia wawekezaji na kupanua fursa za kiuchumi.
Aidha, Mhe. Makame ameongeza kuwa, tayari Serikali ya Mkoa ilishaanza mchakato wa kuanzisha mpango wa maonesho hayo na kwamba pendekezo lililotolewa na wadau wa sekta binafsi kuhusu umuhimu wa jukwaa hilo limeungana na mawazo ya Serikali ya mkoa, hivyo kuwataka wadau kujiandaa kushiriki kikamilifu.
Awali, Mwakilishi wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Songwe, Simon Kitojo, akitoa salamu za chemba hiyo, alishauri mkoa wa Songwe kuwa na maonyesho yatakayokuwa yakihusisha wadau wa sekta za uwekezaji na Biashara ili kuwa kichocheo cha kuongeza ushirikiano baina ya wadau sanjari na kuvutia mitaji mipya kupitia uoneshaji wa bidhaa, ubunifu na fursa za uwekezaji.
