Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WAZIRI KAPINGA AWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI KUBORESHA MAZINGIRA ENDELEVU YA UWEKEZAJI


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb.) amewahakikishia Wawekezaji kuwa Wizara yake itaendelea kuchukua hatua endelevu za kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni ngazi muhimu ya kuendelea kuimarisha na kukuza sekta ya viwanda na biashara nchini kwa kuwa sekta hiyo ina nafasi ya kipekee katika kuchochea ajira.

Vilevile, ameihakikishia Bodi Uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi watoa Huduma kwa Wawekezaji kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uanzishaji uendelevu wa viwanda na biashara, kuhamasisha urasimishaji wa biashara pamoja na kuimarisha matakwa ya viwango vya ubora na matumizi ya vipimo sahihi pamoja na ushindani wa haki sokoni.

Waziri Kapinga Ameyasema hayo Novemba 28, 2025 wakati akihutubia katika Hafla ya Uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi watoa Huduma kwa Wawekezaji na Kongamano la Uwekezaji iliyofanyika jijini Dar es Salaam

Katika hatua nyingine Waziri Kapinga ameahidi kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kutoa ushirikiano kwa Bodi hiyo ili kufikia malengo yaliyoainishwa kupitia Dira ya Maendeleo 2050.

Aidha, amesema Wizara yake itaendelea kufanya tafiti za masoko ya kibiashara ili kuleta tija katika uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao kupanua masoko pamoja na kuimarisha ushindani wa bidhaa zetu kitaifa na kimataifa.