Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MFUMO WA MALIPO CIP KURAHISISHA BIASHARA NA CHINA


Serikali imesema inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara nchini ili kupunguza gharama na changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, hususan China.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa uzinduzi wa mfumo wa malipo wa CIP unaotolewa chini ya Benki ya Stanbic , Agosti 12, 2026 jijini Dar es Salaam.

Londo amesema hatua hiyo inatekelezwa kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanawekewa mazingira wezeshi yatakayowawezesha kufanya biashara kwa ufanisi na kutunza fedha zao.

Amesema mfumo huo utawasaidia wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka China kufanya malipo moja kwa moja kwa kutumia Yuan ya China, badala ya kupitia mchakato mrefu wa kubadilisha fedha.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, mfumo huo unatarajiwa kumsaidia mfanyabiashara kupunguza gharama zinazoweza kujitokeza katika ubadilishaji wa fedha na kuhakikisha anapata thamani halisi ya bidhaa anazoagiza.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za fedha na wadau wa sekta binafsi katika kuanzisha mifumo ya malipo itakayorahisisha biashara, kupunguza gharama na kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa Tanzania katika soko la kimataifa.