Habari
SERIKALI YAWATOA HOFU WADAU WA POMBE KALI NCHINI
Serikali imekutana na wamiliki wa viwanda vinavyozalisha pombe kali nchini kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wazalishaji, hususan uwepo wa bidhaa bandia na zisizokidhi viwango.
Kikao hicho kimefanyika Agosti 24, 2026, jijini Dar es Salaam, kati ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), na wamiliki wa viwanda vya pombe kali ili kutafuta suluhu ya changamoto hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kapinga amesisitiza umuhimu wa wazalishaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazohusu uanzishwaji na uendeshaji wa viwanda vya pombe kali kwa kuzingatia ubora, usafi na afya ya mtumiaji.
Amesema wazalishaji wanapaswa kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vya ubora, usafi na usalama wa afya ya watumiaji, huku wakizingatia matakwa yote ya kisheria katika uzalishaji na uuzaji wa bidhaa hizo.
Mhe. Kapinga amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na bidhaa bandia na duni, huku ikilenga kuhakikisha wazalishaji wanaofuata sheria wanafanya biashara katika mazingira rafiki na yenye usawa.
Katika kikao hicho wamekubaliana kuimarisha utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu namna ya kutambua na kutofautisha pombe halali na bidhaa bandia.
Hatua hiyo inalenga kulinda afya na usalama wa watumiaji, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa salama na zenye ubora kwa bei inayokubalika.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali, wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi ili kuhakikisha bidhaa zinazofika sokoni zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
