Habari
SERIKALI YAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TBL, KUKUZA SEKTA YA VIWANDA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Breweries Plc (TBL), Bi. Michelle Kilpin, Agosti 27, 2026 katika Ofisi ya Wizara Jijini Dodoma.
Kikao hicho kimelenga kujadili shughuli zinazofanywa za Kampuni hiyo na mchango wake katika uchumi wa taifa na maeneo ya kuimarisha zaidi katika ushirikiano kati ya TBL na Wizara pamoja na kujitambulisha rasmi kwa Mkurugenzi huyo.
Serikali imeeleza kutambua na kuthamini mchango wa TBL katika uchumi wa taifa kupitia uwekezaji, uanzishaji wa ajira, ulipaji wa kodi na mapato mengine ya Serikali, pamoja na kuunga mkono kilimo cha ndani na minyororo ya thamani inayohusiana na uzalishaji, hatua inayochangia kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Aidha katika kikao hicho Waziri Kapinga amesisitiza umuhimu wa kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na yenye kujenga kati ya Serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kubaini na kutatua changamoto zinazojitokeza, pamoja na kutambua fursa mpya za uwekezaji na upanuzi wa shughuli za viwanda.
Vilevile Kikao hicho kimeonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana na TBL na sekta binafsi kwa ujumla katika kuongeza tija na ushindani wa viwanda, kuimarisha minyororo ya thamani na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika ajira, mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi, sambamba na kuendeleza mageuzi ya Tanzania ya viwanda na kiuchumi.
Kwa upande wa Bodi na Menejimenti ya TBL zimetoa shukrani kwa Wizara na Serikali kwa ujumla kwa juhudi zinazoendelea katika kuunga mkono maendeleo ya viwanda nchini, kuweka mazingira rafiki ya biashara na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.