Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MHE. KATAMBI AIAGIZA CAMARTEC KUIMARISHA TEKNOLOJIA ZA KILIMO NA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAZAO


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi (Mb), amekiagiza Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kuimarisha tafiti, ubunifu na uzalishaji wa teknolojia za kisasa za kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima, kupunguza upotevu wa mazao na kuimarisha uchumi wa taifa.

Ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kituo hicho mkoani Arusha tarehe 23 Desemba 2025, ambapo amesema Serikali inaendelea kukitambua CAMARTEC kama taasisi muhimu katika utekelezaji wa sera za maendeleo ya kilimo na viwanda vinavyotegemea sekta hiyo.

Vilevile, amebainisha kuwa teknolojia zinazobuniwa na kituo hicho zimeleta matokeo chanya kwa wakulima kwa kupunguza utegemezi wa nguvu kazi ya mikono, kuokoa muda na kudhibiti hasara zinazojitokeza wakati wa mavuno na baada ya mavuno.

Aidha, ametaja mashine za kupura mahindi, dengu na maharage pamoja na mashine za kubangua korosho kuwa miongoni mwa bunifu zilizosaidia kutatua changamoto za muda mrefu kwa wakulima wa mazao ya chakula na biashara.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu kilimo kwa kukifanya kuwa shughuli ya kibiashara, ya kisasa na yenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Katambi ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo pamoja na kuimarisha udhibiti wa ubora wa zana za kilimo zinazoingia nchini ili kulinda maslahi ya wakulima.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC Mhandisi. Godfrey Mwinama amesema Menejimenti imepokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri na wapo tayari kuanza kufanya utekelezaji kwa maslahi mapana na ustawi wa Tanzania katika sekata ya Viwanda na Biashara.