Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

NAIBU WAZIRI KATAMBI AAGIZA TIRDO KUFUFUA VIWANDA VILIVYOKUFA KUPITIA UTAFITI NA TEKNOLOJIA


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Patrobas Katambi, ameliagiza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kuangalia kwa kina namna ya kufufua viwanda vilivyokufa na kutoa ushauri wa kitaalamu ili virejee katika uzalishaji.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika shirika hilo Desemba 22,2025 Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kero kubwa kwa wananchi ni kuona kiwanda kipo lakini hakifanyi kazi, ilhali kingeweza kutoa ajira kwa wananchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa uchumi wa nchi.

Amesisitiza kuwa utafiti ni jambo la msingi na nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi nyingi duniani, kwani kupitia utafiti hupatikana taarifa sahihi, iwe ni chanya au hasi, zinazosaidia kupanga na kutekeleza mikakati ya maendeleo.

Aidha amesema tafiti hizo husaidia kufahamu sababu za kiuchumi katika dunia ya leo inayoendeshwa kwa kiwango kikubwa na maarifa na teknolojia.

Mhe. Katambi amesema katika kukuza viwanda na kuzalisha bidhaa zenye ubora, Serikali inalitegemea TIRDO kutoa ushauri sahihi unaozingatia viwango vya sayansi na teknolojia ambapo utasaidia kujenga uhimilivu wa viwanda na kufanikisha matokeo chanya yatakayoviwezesha kushindana katika masoko.

Ameongeza kuwa utafiti unapaswa kuzingatia thamani ya fedha, uwekezaji wa viwanda na miundombinu, pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha teknolojia, ubunifu na uvumbuzi kama vipaumbele vya utafiti ili kukuza fursa za ajira, upatikanaji wa mitaji na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

“Kushindana ni lazima tufanye tafiti tukitambua kuwa wapo wengine wanaoshindana nasi. Tutambue vikwazo, tujifunze kwa waliofanikiwa, tutambue mipaka yetu na tuwe taifa makini lenye mapinduzi ya viwanda,” amesema Katambi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi (DED), Ramsons Mwilangali akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema shirika hilo linaendelea kusaidia sekta ya viwanda nchini kwa kufanya tafiti za teknolojia zinazofaa, kusimamia na kusambaza matokeo ya tafiti kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.