Habari
Dkt.Hashil Abdalah amepokea Tuzo iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt.Hashil Abdalah amepokea Tuzo iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Tuzo hiyo imetolewa na Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kumi wa Wadau wa Lishe uliofanyika Oktoba 2-3, 2024 jijini Mwanza.
Wizara ya Viwanda na Biashara ni moja ya Wizara za kisekta zinazotekeleza Mpango wa Pili Jumuishi wa Lishe ( NMNAP II 2021/2022-2025/2026) katika mpango huo Wizara inajukumu la kuweka mazingira wezeshi ya Biashara kwa wanowekeza kwenye chakula na lishe.
Pia Wizara ina jukumu la kusimamia suala la uongezaji virutubishi kwenye chakula ( unga wa ngano, unga wa mahindi, mafuta ya kula na chumvi) yaani 'food fortification'.
Katika kutekeleza hayo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imerahisisha upatikanaji wa Teknolojia za kuongeza virutubishi kwa wasindikaji wadogo wa chakula ( dossifiers).
Teknolojia hizi kwa sasa zinasambazwa na kampuni ya SANKU ambapo tayari wamefikia Halmashauri 148.
Aidha, Teknolojia hizi zinasambazwa na taasisi ya SIDO kwa kushirikiana na GAIN.Wizara imendaa kanuni za kuongeza virutubishi kwenye chakula yaani 'food fortification regulation', kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji kwenye uzalishaji wa virutubishi.
Kwa sasa Tanzania tunakiwanda cha kuzalisha virutubishi kinachomilikiwa na kampuni ya SANKU kilichozinduliwa na Mhe. Kassim Majaliwa ( Mb.) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania June 15, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Kiwanda hiki kinawezesha upatikanaji wa virutubishi kwa urahisi na kinasaidia wananchi kupambana na udumavu na utapiamlo.