Habari
MAWAZIRI WA NCHI 8 ZA EAC WAKUTANA TANZANIA KUJADILI NAMNA YA KUONDOA VIKWAZO VISIVYO VYA USHURU (NTBS)
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) ameshiriki Mkutano Maalumu wa 59 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Machi 5, 2026 jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika Machi 7, 2026 jijini Arusha, Tanzania.
Mkutano huo umeongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Waziri anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki nchini Kenya, Mhe. Beatrice Askul Moe.
Moe amesema kuwa ajenda zilizoandaliwa zitatoa mwelekeo mpya wa utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya hiyo.
Miongoni mwa ajenda zinazotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huo wa 25 wa Wakuu wa Nchi ambao ndio chombo cha juu cha maamuzi ndani ya Jumuiya hiyo ni pamoja na maendeleo ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC na kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya ushuru (Non-Tariff Barriers – NTBs).
Kwa sasa, Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi wanachama nane ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia, ikiwa na jumla ya idadi ya watu inayokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 300 na pato la pamoja la uchumi (GDP) linalokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 300.
