Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SEKTA YA HUDUMA KUCHOCHEA BIASHARA TANZANIA NA NCHI WANACHAMA WA SADC


Sekta ya huduma imetajwa kuwa nguzo muhimu ya kukuza uchumi ndani ya Tanzania na Ukanda wa nchi wanachama wa SADC ambapo maboresho ya sera ni lazima ili kuondoa vikwazo vya kibiashara,hatua ambazo zinalenga kuongeza ushindani wa kikanda nili kunufaika na fursa za itifaki ya huduma ya SADC.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) Dkt. Latifa Khamis akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Judith Kapinga (Mb), katika Ufunguzi wa Jukwaa la 49 la Majadiliano ya Biashara ya SADC kuhusu Huduma Machi 05,2026 Jijini Dar es Salaam. Ambapo amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetekeleza mageuzi makubwa ya kurahisisha taratibu za udhibiti na kuimarisha mazingira ya uwekezaji hususan sekta za mawasiliano, usafirishaji, na fedha, na uwekezaji mkubwa ukielekezwa kwenye miundombinu ya kidijitali ili kukuza huduma za kisasa ili kuleta muunganiko.

Dkt. Latifa amesema Sekta ya huduma imekuwa muhimu ikichangia zaidi ya nusu ya Pato la Taifa katika nchi nyingi za SADC huku takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la ajira Tanzania kutoka 26.2% (2023) hadi 35.5% (2024), jambo linaloakisi mabadiliko ya kiuchumi hasa kwa vijana na wanawake katika maeneo ya mijini yenye uhitaji wa wataalamu.

Aidha Dkt. Latifa amesema Kundi la vijana limeonekana kuchangamkia fursa za kidijitali kama uhandisi wa kompyuta na teknolojia ya ili kukuza uchumi wa kikanda ambapo hiyo ni fursa kwa SADC kwani asilimia 70 ya watu Afrika ni umri chini ya miaka 30 hali inayochochea ubunifu.

Ameongeza kuwa maendeleo yamefikiwa katika mapitio ya mikataba ya utambuzi wa kitaalamu (MRAs) hasa wahandisi na wahasibu na kusisitiza kuwa kukamilika kwa mikataba kutasaidia wataalamu hao kutambulika na kufanya kazi kwa urahisi zaidi ndani ya SADC kwa kushirikiana na sekta binafsi na kupunguza changamoto za kibiashara

Pia ametoa wito wa kuimarisha uwazi wa kutoa leseni na kuondoa vikwazo vya kisheria kuhusu huduma mipakani na kusema Tanzania iko tayari kushirikiana nchi wanachama ili manufaa ya biashara ya huduma yawafikie wananchi.