Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt. Kijaji: Uwekezaji, Vwanda na Biashara ndio msingi wa maendeleo wa Taifa lolote Duniani


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo katika kuendeleza sekta ya uwekezaji na biashara nchini.

Amesema hayo wakati wa Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es salaam, Januari 02,2023

Akiongea katika mkutano huo, Waziri amesema Serikali imeamua kuboresha mazingira ya Sekta binafsi ili kukuza mchango katika pato la taifa na kwamba ni wakati sasa wa wadau wote wa Sekta binafsi kutoa ushirikiano kwa kuwa wawazi, waadilifu, wakweli, wawajibikaji na wazalendo hasa wanapoombwa taarifa na Serikali.

“Kutokana na majadiliano yetu ya hapa leo, sote tunakiri uwekezaji, viwanda na biashara ndio msingi wa maendeleo wa taifa lolote Duniani hivyo ni muhimu tukaendelea kuimarisha, kama waziri mwenye dhamana, nawaahidi kwamba nimepokea michango yenu yote na kwamba nitaenda kusimamia na kutekeleza yote yanayowezekana na nawakaribisha milango iko wazi muda wowote, tuendelee kushirikiana,” alisema Dkt. Kijaji.

Alisema Sekta ya Umma na Sekta Binafsi zinategemeana na kwamba serikali itaanza kwa kuangalia sera, sheria,  kanuni na  taratibu ili kuingia kwenye utekelezaji wa azimio kubwa lililoamuliwa na kikao hicho la Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji na kuwahakikishia wajumbe namna bora ya kushughulikia mambo yote waliyoyawasilisha kupitia Kamati za Kitaalamu chini ya Baraza la Biashara la Taifa TNBC).

Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe zilizowasilishwa katika majadiliano hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Lawrence Mafuru alisema kuna faida zaidi ya wafanyabiashara wadogo kujiweka kwenye mfumo rasmi ikiwemo kupata fursa za mikopo na kutambulika na Serikali ambapo ni rahiusi kuwekewa mazingira rafiki ya kazi zao kuliko kutojiweka wazi.