Habari
TANZANIA NA ZAMBIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KURAHISISHA BIASHARA NA USAFIRISHAJI WA MIZIGO
📌 Wawakilishi kutoka nchi hizo mbili wakutana Tunduma kujadili changamoto zinazokwamisha biashara na usafirishaji katika mpaka wa Tunduma–Nakonde;
📌 Msongamano wa magari ya mizigo, ucheleweshaji wa uondoshaji wa mizigo na gharama za usafirishaji ni miongoni mwa changamoto zinazolengwa kutatuliwa;
📌 Kikao kinalenga kuweka mapendekezo ya pamoja yatakayobainisha hatua za utekelezaji, taasisi zinazowajibika na muda wa utekelezaji.
TUNDUMA, SONGWE
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia zimekutana katika Kituo cha Pamoja cha Huduma za Mipakani cha Tunduma (Tunduma–Nakonde One Stop Border Post – OSBP), Mkoa wa Songwe, kwa ajili ya kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuondoa Vikwazo Visivyo vya Ushuru (Non-Tariff Barriers – NTBs) vinavyoathiri biashara na usafirishaji wa mizigo kati ya nchi hizo mbili.
Kikao hicho cha pamoja cha siku mbili, kinachofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 5 Novemba 2026, kinaongozwa na Bw. Ombeni Mwasha, Mkurugenzi wa Idara ya Mtangamano wa Biashara katika Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania, kwa kushirikiana na Dkt. Simon Ng’ona, Mkurugenzi wa Biashara ya Nje katika Wizara ya Biashara na Mauzo ya Nje ya Zambia (Director of Foreign Trade, Ministry of Trade and Exports).
Kikao hicho kinafanyika kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika kubaini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokwamisha biashara na usafirishaji wa mizigo kupitia mpaka wa Tunduma–Nakonde na Ushoroba wa Kati kwa ujumla. Aidha, kikao hicho kinatoa fursa ya kupitia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tano wa Kamati ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika Mei 2025.
Miongoni mwa changamoto zinazojadiliwa ni msongamano wa magari ya mizigo katika Kituo cha kutolea Huduma kwa Pamoja Mpakani Tunduma, ucheleweshaji wa uondoshaji wa mizigo, gharama kubwa za usafirishaji, upungufu wa miundombinu na miundo mbinu duni pamoja na changamoto za uratibu wa shughuli za taasisi zinazotoa huduma mipakani.
Katika kikao hicho, sekta binafsi zinapata nafasi ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili wadau wa usafirishaji kupitia vyama vya wasafirishaji na Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) na Zambia (TA-Zambia), pamoja na vyama vya Mawakala wa Forodha. Aidha, wasimamizi wa vituo vya mipakani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) wanawasilisha taarifa za utendaji wa vituo vya Tunduma na Nakonde kwa ajili ya kupitia ufanisi wa mifumo inayotumika katika Kituo hicho cha Pamoja cha Huduma za Mipakani (OSBP).
Matokeo yanayotarajiwa kutokana na kikao hicho ni kuandaliwa kwa mapendekezo ya pamoja ya utekelezaji yatakayobainisha hatua za kutatua changamoto zilizojitokeza, taasisi zinazohusika na muda wa utekelezaji. Hatua hiyo inalenga kupunguza muda na gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa huduma za mipakani na kuimarisha ushindani wa Ushoroba wa Kati, hatua itakayochangia kukuza biashara kati ya Tanzania, Zambia na nchi nyingine zinazotumia ukanda huo.
