Habari
WAZIRI MKUU AZINDUA SERA YA MAENDELEO ENDELEVU YA VIWANDA, JASIRIAMALI NDOGO NA ZA KATI
📌Ameitaka Wizara kuandaa mikakati ya kutekeleza sera zote na kufanya tathmini na ufuatiliaji;
📌Awataka watanzania kuwa wazalendo na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini;
📌Waziri kapinga asema mafanikio ya Sera mpya yatapimwa kwa idadi ya biashara zinazokua kutoka ndogo kwenda kubwa;
Dodoma
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba Leo tarehe 04 amezindua rasmi Sera ya maendeleo Endelea ya viwanda na Sera ya maendeleo ya jasiriamali ndogo na za Kati mjini Dodoma na kuitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuandaa mikakati ya kutekeleza Sera zote sambamba na kufanya tathmini na ufuatiliaji.
Mheshimiwa Mwigulu amewataka watanzania kujiamini na kuwa wazalendo kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kulinda bidhaa zinazozalishwa kwenye viwanda vyetu kwani vitasaidia kuleta ajira na kuongeza pato la Taifa.
Alisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kupata bidhaa zinazozalishwa nchini katika ujenzi, ununuzi wa samani na mahitaji mengine, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukuza viwanda, kulinda ajira na kuongeza mapato ya Taifa.
“jambo hili lianzie serikalini kwakuwa serikalini inajenga majengo hivyo bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zitumike hapa nchini’’Alisema Mhe Mwigulu
ametaja vioo, nondo, marumaru na samani kuwa miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa nchini ambazo taasisi za umma zinapaswa kutumia huku akisisitiza kuwa Serikali lazima iongoze kwa vitendo katika kutekeleza sera inazozitunga..
Aidha, Waziri Mkuu ametaka sheria ziangaliwe na kurekebishwa iwapo zina mianya inayokwamisha matumizi ya bidhaa za ndani au kutoa nafasi ya kukwepa utekelezaji wa maelekezo hayo.
Amesema jitihada za kujenga viwanda haziwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa ikiwa bidhaa zinazozalishwa hazitumiki, kwa kuwa kukosekana kwa soko kunapunguza uzalishaji, ajira na mapato.
“Tutumie bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kujiamini, kufurahia na kujivunia, ili kulinda viwanda vyetu, ajira na mapato ya nchi yetu, pamoja na kukuza uchumi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amewataka watendaji wa Serikali kubadili mtazamo kuhusu sekta binafsi na kuitambua kuwa mshirika muhimu katika kujenga uchumi unaojitegemea.
Amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mitaji na uwekezaji, pamoja na kuendeleza mazingira yanayoiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Kuhusu utekelezaji wa sera zilizozinduliwa, Dkt. Mwigulu ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara kuandaa mikakati thabiti, kufanya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kushirikiana na wizara za kisekta na sekta binafsi kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Pia, ameitaka wizara kusimamia na kuratibu minyororo ya thamani ili kuwezesha jasiriamali ndogo na za kati kuzalisha malighafi na kutoa huduma zinazohitajika viwandani.
Alisisiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuboresha miundombinu ya nishati, maji, barabara na reli ili kuongeza uwezo wa viwanda kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema wizara imeandaa mkakati wa utekelezaji wa miaka kumi wenye shabaha za kila mwaka, ambazo zitafuatiliwa na kutathminiwa ili kuhakikisha sera hizo zinaleta matokeo.
Amesema utekelezaji huo utawapa nafasi jasiriamali ndogo na za kati na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan katika masoko ya kikanda na Afrika.
Waziri Kapinga amesema uchumi wa dola trilioni moja utafikiwa iwapo mageuzi kwenye sekta ya viwanda yatachochea ukuaji wa uchumi
Aidha amesema maono ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuona sekta ya viwanda inakua na kuchangia kwenye Pato la Taifa
Katika hafla hiyo Wizara ya viwanda ilitoa tuzo kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa anaouyoa kuwezesha mageuzi kwenye sekta ya viwanda sambamba na mgeni rasmi kwa kukubali kushiriki hafla ya uzinduzi.
