Habari
LONDO: SERIKALI KUENDELEA KUTENGA MAENEO KWA AJILI YA VIWANDA VIDOGO NA VYA KATI
📌 SIDO yaendeleza maeneo ya viwanda kwa wastani wa asilimia 27 ili kuongeza fursa za uzalishaji kwa wajasiriamali.
📌 yatenga takribani ekari 898 katika mikoa 26 nchini kwa ajili ya shughuli za wajasiriamali.
📌 Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wanawake wajasiriamali kupata maeneo, mitaji na kushiriki katika uwekezaji.
DODOMA.
Serikali imesema itaendelea kutenga na kuendeleza maeneo maalumu kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo na vya kati ili kuwawezesha wajasiriamali, wakiwemo wanawake, kupata maeneo rasmi ya kufanyia shughuli za uzalishaji na biashara.
Akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Janeth Elias Mahawanga kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Bungeni jijini Dodoma Novemba 3, 2026, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amesema Serikali inaendelea kuhamasisha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati.
Mhe. Londo amesema Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) inaendelea kutenga na kuendeleza maeneo yatakayotumiwa na wajasiriamali wadogo na wa kati kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.
Amesema hadi Septemba 2026, SIDO ilikuwa imefanikiwa kutenga takribani ekari 898 katika mikoa 26 nchini, huku maeneo hayo yakiwa yameendelezwa kwa wastani wa asilimia 27. Maendeleo hayo yanajumuisha ujenzi wa majengo 467 ya viwanda vidogo na vya kati pamoja na viwanda 3,198.
Akizungumzia suala la wanawake kupata maeneo na haki ya kumiliki ardhi kwa ajili ya uwekezaji, Mhe. Londo amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imejengwa katika misingi ya uchumi imara na jumuishi unaotegemea ushiriki wa wananchi wote katika shughuli za uzalishaji.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupata mitaji, elimu na mazingira rafiki ya kufanya biashara, ikiwemo kushughulikia changamoto zinazohusiana na upatikanaji na umiliki wa ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na taasisi nyingine za Serikali.
Aidha, ameeleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa pamoja na taasisi zake kutenga maeneo na kuimarisha miundombinu rafiki kwa wajasiriamali, ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara na uzalishaji na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
