Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dkt.Philip Mpango ametoa rai kwa wamiliki na wazalishaji wa bidhaa za viwandani kuongeza wigo wa uwekezaji wa viwanda


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Mpango ametoa rai kwa wamiliki na wazalishaji wa bidhaa za viwandani kuongeza wigo wa uwekezaji wa viwanda vya kimkakati vinavyozalisha bidhaa za kati hasa vile vinavyozalisha ajira kwa wingi, kuchochea ubunifu, tija na vyenye uhusiano na sekta nyinginezo.

Dkt.Mpango ametoa rai hiyo wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za 18 za Rais za Mwaka kwa Wazalishaji Bora zinazofahamaika kama (PMAYA) iliyofanyika katika Ukumbi wa Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais Dkt.Mpango amewasisitiza sekta ya Viwanda na wazalishaji Kuingi ubia na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili kuanzisha vituo atamizi Vya sayansi na teknolojia na uvumbuzi ili kuleta na kupata teknolojia zinazochipukia na kuwaunganisha wavumbuzi wa teknolojia Duniani na wazalishaji hapa nchini.

Aidha Dkt.Mpango ametoa wito kwa wazalishaji na Sekta Binafsi kutumia nguvu kazi kubwa ya vijana pamoja na kuanza kuwapatia fursa zaidi za mafunzo ya vitendo kazini ili kuongeza ujuzi wao na kuwadhamini .

Pamoja hayo Dkt. Mpango ameiagiza CTI kuanza kuratibu na kuwatumia wazalishaji wa viwandani waliofanikiwa kutoa mafunzo kwa wanafunzi vyuoni.

Nae Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe(Mb) amesema kuwa Wizara imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Sita la kuendeleza sekta ya Viwanda linafanikiwa ikiwemo kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara (MKUMBI), kufanya mapitio ya sera za kusimamia viwanda na biashara pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya vya aina zote kwenye Mikoa na Wilaya zote nchini.

Vile vile Mhe.Kigahe amewahimiza wadau wote wa viwanda kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya kutumia fursa za biashara zitakazotokana na Eneo Huru la Biashara la (African Continental Free Trade Area (AfCFTA) kwani Wizara imekamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika mwaka 2023 kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini