Habari
WAZIRI KAPINGA: SABASABA YAFUNGUA MILANGO YA MASOKO YA KIMATAIFA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe.Judith Kapinga (Mb), amesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuwa chachu ya kukuza biashara, uwekezaji na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kikanda na kimataifa.
Akizungumza Julai 03, 2026 wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya 50 ya Sabasaba, Waziri Kapinga amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yanaonesha ukuaji mkubwa wa maonesho hayo, huku mauzo ya papo kwa papo yakiongezeka kutoka Sh. Bilioni 2.4 mwaka 2021 hadi Sh. Bilioni 7.06 mwaka 2025.
Amesema idadi ya waoneshaji wa ndani imeongezeka kutoka 2,926 hadi 3,670, huku ushiriki wa kimataifa ukikua kutoka kampuni 76 za nchi 17 hadi kampuni 430 kutoka nchi 30, jambo linaloifanya DITF kuwa miongoni mwa maonesho makubwa barani Afrika.
Kapinga amesema maonesho hayo yanaakisi maendeleo ya uchumi wa Tanzania na uwezo wa nchi kuzalisha bidhaa zenye ubora zinazoweza kushindana katika masoko ya dunia.
Ameeleza kuwa kupitia diplomasia ya uchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imefanikiwa kufungua masoko mapya, kuvutia wawekezaji na kuimarisha biashara ya kimataifa.
Amebainisha kuwa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yamefikia dola za Marekani bilioni 17, huku mauzo ya bidhaa pekee yakivuka dola bilioni 10. Aidha, mauzo ya dhahabu yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 35 na kufikia dola bilioni 4.4, wakati sekta za kilimo, viwanda, utalii na usafirishaji zikiendelea kuchangia ukuaji wa uchumi.
Kapinga amesema kuelekea mwaka 2050, Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TANTRADE imejipanga kuifanya Sabasaba kuwa jukwaa kuu la kimataifa linalounganisha biashara, teknolojia na uwekezaji, huku likiongeza mauzo ya bidhaa zenye chapa ya Made in Tanzania na kutumia kikamilifu fursa za Soko Huru la Afrika (AfCFTA).
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania duniani.
