Habari
RAIS DKT. SAMIA AIPONGEZA TANTRADE KWA MABORESHO ENDELEVU YA MAONESHO YA SABASABA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha na kuendeleza Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akibainisha kuwa mabadiliko yanayofanyika kila mwaka yameendelea kuongeza hadhi, ubora na mvuto wa maonesho hayo.
Akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa Maonesho ya 50 ya Sabasaba, Mhe. Dkt. Samia alisema maboresho yanayofanywa na TanTrade yamechangia kuvutia washiriki na wageni wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi, huku yakiongeza fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi. Alisisitiza kuwa maendeleo hayo yanaonesha dhamira ya TanTrade ya kuhakikisha maonesho yanaendana na mahitaji ya wakati na ushindani wa kimataifa.
Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia aliitaka TanTrade kuendelea kubuni na kutekeleza mikakati ya ubunifu itakayozidi kuimarisha Maonesho ya Sabasaba kama jukwaa kuu la biashara nchini na ukanda wa Afrika Mashariki. Alieleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na kuiwezesha TanTrade ili maonesho hayo yaendelee kuwa chachu ya maendeleo ya biashara, viwanda na uchumi wa Taifa.
