Habari
DKT. ABDALLAH: FCC YAJIDHATITI KULINDA HAKI ZA WALAJI NA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kulinda haki za walaji na kudhibiti bidhaa bandia kupitia Tume ya Ushindani (FCC) ambayo ina mchango mkubwa katika kukuza viwanda nchini na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora, salama na zenye bei stahiki.
Akizungumza jijini Tanga wakati akifungua Semina ya Uhamasishaji wa Masuala ya Ushindani, Ulinzi wa Mlaji na Udhibiti wa Bidhaa Bandia iliyofanyika katika ukumbi wa The New Kiboko, Tanga Ltd Oktoba 15,
2025, Dkt. Abdallah alisema semina hiyo imelenga kuongeza uelewa wa watendaji katika kuhakikisha masoko nchini yanabaki na ushindani wa haki unaowezesha maendeleo endelevu ya sekta ya viwanda na biiashara.
Aidha, Dkt. Abdallah alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miongozo yake ya kukuza sekta ya viwanda na biashara huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ushindani yanayochochea ubunifu na ukuaji wa sekta ya viwanda.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema Tume Hiyo inaendelea kufanya doria na ukaguzi katika masoko kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakidhi viwango na hadhi ya soko na kupunguza bidhaa bandia na kulinda afya na maslahi ya walaji.
Naye, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Sempeho Manongi, amesem kuwa mafunzo hayo yatasaidia Menejimenti ya Wizara na FCC kuelewa kwa kina sheria za ushindani, ulinzi wa mlaji na mbinu za kudhibiti bidhaa bandia katika mazingira ya sasa ya biashara ya kidijitali.
Vilevile, Mkurugenzi wa Tafiti Muungano ya Makampuni na utoaji wa elimu Bi. Zaituni Kikula amesema, ni muhimu kwa Menejimenti ya Wizara kujua sheria zinazohusiana na majukumu makubwa ya FCC katika kuhakikisha Soko linaimarika na walaji wanapata bidhaa sahihi
ili kusimamia vyema taasisi zake na kutoa ushauri wa kisera unaozingatia maslahi ya walaji na maendeleo ya sekta.
