Habari
DKT. HASHIL AZINDUA ZOEZI LA KUAINISHA VIWANDA, RASILIMALI ARUSHA NA MANYARA
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amesema zoezi la Utambuzi wa taarifa za viwanda na Wajasirimali ni fursa kwa Serikali kubaini fursa za uwekezaji na biashara ikiwemo utambuzi wa viwanda na malighafi zinazotumiwa na kiwango cha ajira wanachozalisha.
Ameyasema hayo Novemba 17, 2025 Jijini Arusha wakati wa hafla ya uzinduzi wa zoezi la utambuzi wa viwanda, rasilimali na fursa za uwekezaji katika Mkoa wa Arusha na Manyara linaratibiwa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI
Aidha Dkt. Hashil amesisitiza Kuwa lengo kubwa la zoezi hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona uchumi wa viwanda nchini Tanzania unakua kwa kufanya utafiti ili kuwezesha ajira, uwekezaji na wazawa kubaini fursa za kuanzisha viwanda na uwekezaji katika mikoa mbalimbali kupitia taarifa sahihi za viwanda.
Dkt. Hashil amesisitiza kuwa Serikali imejipanga vema katika kuhakikisha changamoto ya ajira kwa vijana , wanawake na makundi maalum zinaondoka kwa kubaini viwanda vinavyofanya kazi na visivyofanya kazi, fursa za uwekezaji kwa mikoa ya Arusha na Manyara huku mikoa mingine ikifuatia.
Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO Prof. Madundo Mtambo amesema baada ya ukusanyaji wa taarifa za viwanda hivyo nchi nzima Serikali itaziweka katika Mfumo wa Utoaji wa Taarifa za Viwanda (NIIMS) ambapo zoezi hili muhimu litarahisisha katika kutoa taarifa, kutunga sera, kupanga mipango ya maendeleo na ufuatiliaji wa sekta hiyo.
Nao Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa na Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Mariam Muhaji wamesema zoezi hilo litaiwezesha Serikali kubaini takwimu sahihi za viwanda kupitia mfumo maalum ili kubaini fursa za uwekezaji na uanzishaji viwanda, malighafi zinazotumiwa na ubora wake huku Viwanda hivyo vikiongeza ajira, Pato la Taifa na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Jumanne John kutoka Manyara amesema zoezi hilo la utambuzi wa viwanda na uwekezaji litasaidia Serikali kukuza uchumi na upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kwa kila mkoa.
