Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT. HASHIL AISISITIZA BRELA KUTOA MAFUNZO KWA WATUMISHI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah ameisisitiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutoa mafunzo endelevu watumishi wa Wizara na Taasisi zake kwa lengo la kujenga uwezo na kuongeza ufanisi, uwajibikaji, ubunifu na ufuatiliaji katika sekta ya viwanda na biashara na kuleta mchango chanya katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Ameyasema hayo Novemba 13, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Viongozi na Watumishi wa Wizara kuhusu mifumo na huduma zinazotolewa na BRELA yaliyolenga kuwajengea uelewa wa kina ili kuhakikisha huduma za usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, utoaji wa leseni za biashara na leseni za viwanda, matumizi ya mifumo ya kidijitali ya BRELA na huduma za ulinzi wa haki miliki za ubunifu zinatolewa kwa ufanisi, uwazi, na kwa viwango vya kimataifa.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt Suleiman Serera amesema mafunzo hayo muhimu yanayoelekeza Washiriki kujifunza huduma na mifumo hiyo yataimarisha misingi ya utoaji ushauri wa kitaalamu wenye tija kwa wawekezaji, wafanyabiashara, na wananchi wanaohitaji huduma kutoka Serikalini.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri – BRELA Prof. Neema Mori, amesema BRELA inasimamia Sheria sita (6) ambazo ni Sheria ya Kampuni Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, Sheria ya Alama za Biashara na Huduma, Sheria ya Hataza, Sheria ya Usajili na Leseni za Viwanda na Sheria ya Leseni za Biashara ili kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanakuwa ya wazi, salama, na yanayozingatia misingi ya kisheria, huku ikichangia moja kwa moja katika juhudi za Serikali za kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wa biashara za ndani na nje ya nchi.

Awali, akiwasilisha taarifa ya mafunzo hayo kwa Katibu Mkuu, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu ya kina kuhusu mamlaka, mifumo ya kidijitali, na huduma kuu zinazotolewa na BRELA ili kuhakikisha washiriki hao wanafahamu kwa undani majukumu ya BRELA na wawe mabalozi wazuri wa kutoa ushauri sahihi, wa kitaalamu, na wa haraka kwa Wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi.