Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT. MWIGULU ATAKA ASILIMIA 20 YA MAPATO YA MAZAO IELEKEZWE KUJENGA MAGHALA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano waTanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema asilimia 20 ya mapato yatokanayo na mazao ya kilimo inapaswa kuelekezwa katika ujenzi wa maghala karibu na maeneo ya uzalishaji ili kupunguza gharama kwa wakulima na kuongeza ufanisi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini.

Waziri Mkuu amesema hayo Mei 19, 2026 jijini Dodoma wakati alipokuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) yenye kaulimbiu isemayo “Mfumo Imara, Uchumi Endelevu.”

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu pia alizindua rasmi Mkakati wa Uhamasishaji wa Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaolenga kuongeza uelewa na ushiriki wa wakulima, wafanyabiashara, vyama vya ushirika, taasisi za fedha pamoja na wadau wengine katika matumizi ya mfumo huo nchini.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuimarisha mfumo huo kwa kuwa umechangia kuongeza uwazi na ushindani katika biashara ya mazao pamoja na kuhakikisha wakulima wananufaika na thamani halisi ya mazao yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na taasisi za fedha inaandaa utaratibu wa kuwawezesha wakulima kupata malipo ya awali kupitia mazao yaliyohifadhiwa ghalani ili kuwaondoa katika changamoto ya kukopwa mazao au kuuza kwa hasara.

Pia amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu mali zinazohamishika kutumika kama dhamana ikiwemo stakabadhi za ghala.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesisitiza matumizi ya vipimo rasmi na vifungashio vinavyokidhi viwango huku akieleza kuwa matumizi ya “lumbesa” hayapaswi kuendelea katika biashara ya kisasa ya mazao.

Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Judith Kapinga amesema mafanikio ya miaka 20 ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yametokana na uwekezaji na usimamizi madhubuti unaoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya WRRB, Bi. Geraldine Rasheli amesema mfumo huo umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha biashara ya mazao, kuongeza uwazi wa masoko na kuwawezesha wakulima.