Habari
DKT. SAID ATOA WITO KWA WATANZANIA KUTUMIA BIDHAA ZA NDANI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Said Seif Mzee, ametoa wito kwa Watanzania kutumia vifaa vinavyozalishwa na viwanda vya ndani ili kupunguza gharama za kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Dkt. Said ametoa wito huo Oktoba 19, 2025, alipotembelea Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) jijini Arusha na Kiwanda cha KMTC Manufacturing Limited kilichopo mkoani Kilimanjaro, ambapo alipata fursa ya kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa katika viwanda hivyo.
Kwa upande wake, Dkt. Abdulla Rashid Abdulla, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda katika Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amesema CAMARTEC itasaidia kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia uzalishaji na matumizi ya teknolojia endelevu, hususan katika ukaushaji wa dagaa na zao la mwani.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mohamed Dhamir Kombo ameishauri CAMARTEC kushirikiana na Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima katika mashamba yao.
Ujumbe huo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umemaliza rasmi ziara ya siku mbili iliyoanza Oktoba 18, 2025, ambapo pande zote mbili ziliahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala ya teknolojia na maendeleo ya viwanda.
