Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DK. SULEIMAN SERERA AWATAKA WATUMISHI HOROHORO KUFANYA KAZI KWA UADILIFU, APONGEZA FCC KWA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Selemain Serera, amewaagiza watumishi wa Kituo cha Forodha cha Horohoro, kilichoko Mpakani mwa Tanzania na Kenya, kufanya kazi kwa uadilifu na nidhamu ya hali ya juu wakati wa utoaji wa huduma.

Ametoa maagizo hayo Oktoba 16, 2025 wakati wa ziara ya Menejimenti ya Tume ya Ushindani (FCC) na Menejimenti ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika Kituo cha Forodha Horohoro Mpakani mwa Tanzania na Kenya ikiwa ni muda mfupi baada ya kuzuru Bandari ya Tanga ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha semina ya siku mbili iliyolenga kuimarisha uelewa wa masuala ya ushindani, kulinda walaji na kudhibiti bidhaa bandia.

Dkt. Suleiman Serera ameeleza kuwa Kituo cha Forodha cha Horohoro kinahudumia watu wa ndani na nje ya nchi, na hivyo ni muhimu kwa watumishi kutekeleza wajibu wao kikamilifu huku akibainisha kuwa Serikali ina imani na weledi wa watumishi, na kutahadharisha kuwa uwepo wa wachache wasio waadilifu unaweza kuharibu sifa na ubora wa huduma zinazotolewa.

Kuhusu juhudi za Serikali Dkt. Suleiman Serera alisema "Tupo kwa ajili ya kuchagiza nguvu na jitihada kubwa ambazo mnazofanya. Kama kuna mambo yatakuwa na changamoto tutayachukua kwenda kuyafanyia kazi,"

Katika hatua nyingine, Dkt. Serera alipongeza jitihada za watumishi hao kwa kuendelea kuongeza mapato ya nchi na kuwasisitiza umuhimu wa kuendelea kuangalia namna ya kudhibiti upitishaji bidhaa kimagendo ili kulinda usalama wa Watanzania na maslahi ya nchi kwa ujumla.

Akizungumza kwa upande wa Tume ya Ushindani (FCC), Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Khadija Ngasongwa, alisema FCC imejikita katika kudhibiti bidhaa bandia kuingia nchini kwa kuangalia alama ya bidhaa ili kuonesha mahali ilipotoka na uhalisia wake. Alibainisha kuwa FCC inajipanga kuweka mikakati ya kuweka ofisi mikoani kupitia mfumo wa TRA wa Tanoga unaohusisha taasisi za ukaguzi ambazo hazina mifumo yao ya ndani.