Habari
WAFANYABIASHARA WANAOSAFIRISHA BIDHAA CHINA KUWEZESHWA
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), ameziagiza Taasisi za Serikali Kuwa Wawezeshaji na si Wadhibiti katika kuwawezesha Wafanyabiashara wanaosafirisha Bidhaa nje ya Nchi hususani China, Ili kuwainua kiuchumi, na kuwaondolea vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha shughuli zao.
Waziri Kapinga ameyasema hayo, Mei 09, 2026, jijini Dar es Salaam katika Hotel ya Johari Rotana, wakati wa Mkutano wa Wadau kuhusu Fursa ya Kuuza Bidhaa katika Soko la China bila Ushuru (Zero Tariff) ikiwa no utekelezaji wa mikakati ya kushirikiana na wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi,
Aidha, amesisitiza kuwa Wizara yake iko tayari kutoa wataalamu watakaosaidia kufanikisha biashara hizo, huku akibainisha kuwa sekta ya kilimo ndiyo muhimili mkuu wa mauzo hayo ya nje ya nchi.
Vilevile amebainisha kuwa Wizara yake imepanga kuanzisha Jukwaa la Wasafirishaji (Exporters Forum) ili kuratibu fursa za kila bidhaa na kuongeza ushindani kwa kuwa sekta binafsi ndiyo Injini ya maendeleo, hivyo mafanikio ya mpango huo yatategemea ubunifu wa wazalishaji katika kuongeza thamani ya bidhaa zao.
Waziri Kapinga pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Diplomasia ya uchumi iliyofungua soko la China, ambalo ni mshirika mkuu wa biashara wa Tanzania.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw. Aristides Mbwasi, amesema Tanzania inashiriki katika mikataba mbalimbali ya masoko ya kikanda na kimataifa kama EAC, SADC, AfCFTA, na sasa fursa ya China, kwa lengo la kuhakikisha bidhaa za ndani zinapata soko la uhakika bila vikwazo vya kodi, jambo litakaloinua thamani ya bidhaa za Kitanzania Kimataifa.
Kwa upande wake Mshauri wa Uchumi Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China Bw. Chu Kun, amesema lengo kuu la sera ya Ushuru wa Sifuri kwa bidhaa zinazotoka katika nchi zilizoendelea kwa kiwango cha chini (LDCs) zenye uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo ni kupunguza gharama za bidhaa za Afrika zinapoingia katika soko kubwa la China, jambo litakaloongeza ushindani wa bidhaa hizo dhidi ya zile za mataifa mengine duniani.
