Habari
SERIKALI YAENDELEA NA MPANGO WA KUANZISHA KONGANI ZA VIWANDA SINGIDA
Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuanzisha Kongani za Viwanda katika wilaya zote nchini, ikiwemo Mkoa wa Singida, kwa lengo la kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Hayo yamesemwa Mei 15, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), akijibu Swali namba 356 la Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida Mhe. Grace Elias Mkoma aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kuanzisha Kongani za
Viwanda kwa Wilaya za Mkoa wa Singida.
Amesema hadi kufikia Desemba 2025, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kuanzisha Kongani 36 za Viwanda katika Mikoa 16 nchini, hatua inayolenga kuongeza uwekezaji wa Viwanda pamoja na kuchochea maendeleo ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Akijibu Swali hilo, Londo amesema tayari maeneo yametengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni Singida Manispaa yenye ekari 8.6, Manyoni ekari 4.7, Iramba ekari 20, Itigi ekari 10 pamoja na Mkalama ekari 10.
