Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YAIGIZA BODI YA MKONGE KUCHUKUA HATUA ZA KISHERIA KWA WAFANYABIASHARA WADANGANYIFU WA ZAO HILO


Serikali yaiagiza Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) kuchukua hatua za kisheria kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya udanganyifu katika masoko ya nje na kuchafua taswira ya nchi na kuwaweka kwwnye mazingira magumu wafanyabiashara wengine wanaofuata taratibu na kufanya biashara kwa uaminifu.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb) wakati wa kikao cha Bodi ya Mkonge, wafanyabiashara wa Mkonge na Chama cha Wakulima wa Mkonge (SAT) katika ukumbi wa mikutano wa Tanga Beach Hotel, Septemba 14,2026 Jijini Tanga ambapo amesema kufanya hivyo kunadhoofisha uaminifu wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Aidha amesema Tanzania inaendesha uchumi wa soko huria, lakini uhuru huo haupaswi kutumiwa kama mwanya wa kufanya biashara kinyume cha sheria au kukiuka misingi ya uaminifu katika masoko ya kimataifa kwani kwa kufanya hivyo inatambulika Tanzania na wala si kampuni ya mfanyabiashara.

Londo ameongeza kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vinavyoweza kulazimisha nchi kutumia muda na rasilimali nyingi kurejesha uaminifu na taswira yake katika masoko ya kimataifa.

Vilevile ameiagiza TSB, kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao hilo, kuchukua hatua mapema dhidi ya vitendo hivyo ili kuzuia kuendelea kuathiriwa kwa soko la mkonge na wafanyabiashara wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TSB, Bw. Saddy Kambona, amesema changamoto hiyo ya udanganyifu ni miongoni mwa mambo aliyokutana nayo wakati wa ziara zake katika masoko ya mkonge duniani.

Hata hivyo akizungumzia uzalishaji wa zai hilo amesema uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 36,000 mwaka 2020 hadi tani 75,000 mwaka 2025.