Habari
LONDO AWATAKA WAFANYABIASHARA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb) amezitaka sekta binafsi na wafanyabiashara kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za Serikali ili kulinda afya na usalama wa Watanzania kupitia kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa nchini.
Mhe. Londo ametoa kauli hiyo alipotembelea ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika mpaka wa Namanga mkoani Arusha, kwa lengo la kujionea utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo Septemba 11,2026 Namanga-Arusha.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa tija, huku wakizingatia viwango na ubora wa bidhaa zinazofika kwa wananchi.
Aidha, amezitaka sekta za umma na binafsi kutoa elimu na ushirikiano kwa wafanyabiashara ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi, akisisitiza umuhimu wa huduma kutolewa kwa wakati.
Londo pia ameipongeza TBS kwa kushirikiana na taasisi nyingine mtambuka katika utoaji wa huduma, akisema ziara hiyo imewapa fursa ya kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhusu namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Amesema maboresho hayo yatasaidia kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
