Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA, TAASISI WEZESHI ZAFANYA TATHMINI YA KATAZO LA BIASHARA 15 KWA WAGENI


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, amefanya kikao kazi na taasisi wezeshi za biashara ikiwemo BRELA, TISEZA, TANTRADE, FCC, TPA, TASAC, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi na Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Uchukuzi pamoja na Halmashauri za Dar es Salaam na Mwanza kwa lengo la kujadili na kufanya maboresho katika utekelezaji wa katazo la biashara 15 ambazo haziruhusiwi kwa wageni nchini Septemba 16, 2026 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Balozi Waziri alisema hatua hiyo imekuja kufuatia maoni na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali, hivyo Wizara imeona umuhimu wa kuyafanyia tathmini ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha utekelezaji unazingatia malengo yaliyokusudiwa.

Balozi Salum amesema mapendekezo ya kikao na tathmini itawasilishwa kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hatua zaidi za na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wake huku akisisitiza kuwa Serikali, kupitia Wizara inalenga kulinda na kuimarisha sekta ya biashara nchini kwa kuweka misingi imara ya kiuchumi na kujenga mazingira wezeshi yatakayowawezesha Watanzania kunufaika na fursa za biashara

Aidha, Balozi Waziri alisisitiza umuhimu wa kuzingatia utu katika utekelezaji wa katazo hilo, akibainisha kuwa pamoja na wajibu wa Serikali kusimamia na kutekeleza sheria, utekelezaji wake unapaswa kufanyika kwa kuzingatia utu na kuepusha usumbufu usio wa lazima kwa wahusika.

Baada ya kukamilika kwa tathmini na majadiliano, kikao hicho kilifikia hatua ya kupitisha mapendekezo yaliyofanyiwa maboresho, ambayo sasa yanawasilishwa kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa ajili ya kutoa mwelekeo wa mwisho kuhusu hatua zinazofuata katika utekelezaji wa katazo hilo.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa utekelezaji wa katazo la biashara 15 unakwenda sambamba na sera, sheria na taratibu za Serikali, huku ukizingatia maslahi ya Taifa na mazingira wezeshi kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara.