Habari
Serikali yatoa miezi mitatu kwa Kiwanda cha Viua Dudu kuanza kazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji kutoka sekta ya Viwanda, Dkt. Adelhemu Meru ametoa agizo kwa Shirika la Maendeleo (NDC) kuhakikisha Kiwanda cha kutengeneza dawa za kuua viluwiluwi wa mbu wanaosababisha malaria kilichopo Kibaha mkoani Pwani kinaanza uzalishaji ifikapo Mei mwaka huu. Akizungumza mara baada ya kutembelea na kujionea hali halisi ya Kiwanda hicho Dkt. Meru amesema ili azma iliyowekwa na Serikali ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa Maralia inafanikiwa ni lazima uzalishaji uanze mapema kama ilivyopangwa. Katibu Mkuu amelitaka Shirika la Maendeleo(NDC), litafute fedha hata kwa kukopa katika mabenki ili kulipa deni la dola za Kimarekani milioni 2.1 la Kampuni ya LABIOFAM kutoka nchini Cuba ikiwa ni ongezeko la gharama kutokana na ujenzi wa kiwanda hicho kuchukua muda mrefu. “Hali hii haikubaliki hatuwezi kuwa kioja, tafuteni fedha hizo dola milioni 1 kwa ajili ya majaribio na dola milioni 1.2 kwa ajili ya mtaji, kwani malengo ya Serikali ilikuwa kiwanda kianze kazi kwa muda uliopangwa ili kiweze kukabiliana na ugonjwa wa Maralia na ziada ya dawa kuuzwa nje ya nchi, hivyo kuweza kufikia malengo yaliowekwa,”alisema dokta Meru. Alisisitiza kuwa Selikali haitatoa fedha yeyote ya ruzuku kwa Kiwanda hicho ili kijiendeshe, na badala yake kinatakiwa kuanza uzalishaji na kujiendesha chenyewe kwa faida. Aidha Dkt. Meru ameiagiza NDC kuhakikisha kuwa mishahara ya wafanyakazi wa kiwanda hicho hailipwi na Shirika hilo kama hivi sasa isipokuwa inalipwa na kiwanda chenyewe kwa maana kinatakiwa kujiendesha kibiashara na soko kubwa lipo ndani na nje ya nchi. Awali akitoa taarifa ya Kiwanda hicho Kaimu Mkurugenzi Mwezeshaji wa Shirika la Maendeleo (NDC) Bw.Goodwill Wanga alimweleza Katibu Mkuu kuwa shughuli za ujenzi na kusimikwa kwa Mitambo katika kiwanda hicho umeshakamilika bado kufanyiwa majaribio na kuanza uzalishaji. “Kiwanda hiki kimeshindwa kuanza kuzalisha bidhaa kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha za kukiendesha pamoja na ongezeko la deni la kampuni ya LABIOFAM linalotokana na kuchelewa kuanza kwa mradi”. Amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo kwa sasa ni kuwa mitambo mingi haifanyi kazi vizuri kama ilivyotarajiwa, hivyo wanatafuta fedha za kurudisha mitambo hiyo katika hali ya kawaida. “Umeme siyo wa uhakika, unakatika mara kwa mara hali hii imesababisha mitambo ya kieletroniki kuaribika hivyo tunatafuta fedha ili kununua mashine zilizoharibika ili iweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa” Alieleza kuwa uzalishaji ukianza kiwandani hapo wanatarajia kutengeneza Mbolea na Bio Products zitakazo wanufaisha Watanzania. Kiwanda cha Viua dudu kibaha kilifunguliwa mwaka jana na Rais Mstaafu Mhe.Jakaya Kikwete lengo la kuanzishwa kiwanda hiki ni kumaliza tatizo la Maralia nchini,kwa sasa kiwanda hiki kimeajiri wafanyakazi 143 wengi wao wakiwa ni vijana wa Kitanzania.