Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KUKIWEZESHA ZAIDI KIWANDA CHA TBPL, MZALISHAJI MKUU WA DAWA ZA KIBAILOJIA BARANI AFRIKA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amesema Serikali itaendelea kukijengea uwezo Kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kinachojihusisha na utengenezaji wa dawa za kibailojia zinazotumika kupambana na mbu katika hatua za awali za ukuaji (kiluilui) na za kilimo kwa ajili ya viwavijeshi vamizi.

Dawa hizo zinazozalishwa kiwandani hapo zinasaidia kupunguza matumizi ya dawa za kikemikali katika kilimo.

Dkt. Hashil ameyasema hayo Oktoba 16, 2025 Kibaha mkoani Pwani wakati wa uzinduzi wa hafla ya kuadhimisha miaka 10 ya kiwanda hicho kilichopo Kibaha.

Aidha, Dkt. Hashil ameongeza kuwa kiwanda hicho ambacho ni cha kwanza kwa ukubwa Afrika na cha pili duniani, kimeonesha mafanikio makubwa, hivyo Serikali itaendelea kukiwezesha ili kiongeze uzalishaji wake.

Amesema mafanikio makubwa yaliyooneshwa na Kiwanda hicho yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 zaidi ya shilingi bilioni 11 zilitolewa

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Rafael Moyes, amesema katika kipindi cha miaka 10, kiwanda kimezalisha lita milioni 1.7 za viuatilifu vilivyotumika nchini na vingine kuuzwa katika nchi saba barani Afrika.