Habari
SERIKALI YATAMBUA SEKTA YA SHEREHE KUKUZA UCHUMI, AJIRA KWA VIJANA NA WANAWAKE
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Judith Kapinga (Mb), amesema sekta ya matukio na biashara za sherehe imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa kwa kuchochea ajira, ubunifu na ukuaji wa biashara ndogo na zakati nchini.
Kapinga ameyasema hayo katika kilele cha Maonesho ya Wafanyabiashara wa Sherehe (Adorable Wedding Trade Fair – msimu wa nane) Aprili 19, 2026 jijini Dar es Salaam.
Aidha, sekta hiyo imekuwa ikitoa maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hasa kwa vijana na wanawake, huku ikiunganisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo utalii, usafirishaji, mavazi na teknolojia ya ubunifu.
Tanzania inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yenye lengo la kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu na kwamba sekta ya huduma kama ya matukio ina mchango mkubwa katika kufanikisha azma hiyo kupitia uzalishaji wa ndani na upanuzi wa soko la ajira.
Kapinga alibainisha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni vijana wenye umri chini ya miaka 35. Hivyo sekta hiyo ni fursa muhimu kwao kujiajiri bila kuhitaji mitaji mikubwa, akiwahimiza kutumia ubunifu na teknolojia kujenga biashara endelevu.
Aidha, amesisitiza mchango mkubwa wa wanawake katika sekta hiyo, akieleza kuwa wao si washiriki tu bali ndio wamiliki wakuu wa biashara nyingi za sherehe, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa mikopo, mafunzo na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Katika hotuba yake, Kapinga alisema Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sera, miundombinu na mifumo ya biashara ili kukuza ushindani na ubunifu, huku ikihamasisha matumizi ya teknolojia katika shughuli za kiuchumi.
Pia ametoa wito kwa wajasiriamali kusajili biashara zao na kuendesha shughuli zao kwa kufuata sheria ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zikiwemo mikopo na ushiriki katika masoko ya kimataifa.
Amewahimisa umuhimu wa ubora wa huduma, ushirikiano wa kibiashara na matumizi ya majukwaa ya kidijitali kama nyenzo muhimu za kuongeza ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
